BABA KIUMBE WA AJABU SEHEMY YA 1 - 10


BABA KIUMBE WA AJABU SEHEMY YA 1 - 10

KUSHINDWA KUNITOA KAFARA KULIMFANYA BABA AGEUKE KIUMBE CHA AJABU
Katika dunia ya Mungu kuna mambo mengi ambayo ukihadithiwa unaweza kudhani ni simulizi za kutunga na za kusisimua. Lakini siku zote kila aisifiaye mvua basi ujue imemnyea. Dunia imezungukwa na siri nzito ndani ya majumba ya watu, kuna mambo mazito ambayo ni chukizo kwa Muumba.
Si kila mwenye maisha mazuri au tajiri mali alizonazo kazipata kihalali. Wengi utajiri wao unatokana na nguvu za giza, utajiri anaoambatana na kutoa kafara ya kitu. Wapo wanaotoa kafara watoto, wake au waume zao, pia wapo wanaowageuza watoto, wake au waume zao kuwa mandondocha kama ‘chuma ulete’ wa kuwaongezea kipato.
Nyumba nyingi huwa na vyumba vya siri ambavyo huwa havifunguliwi kutokana na masharti ya mganga na kufanya watu wabaki na maswali. Pia nyumba nyingine unakuta kuna mtoto ambaye akili zake si nzuri, akikaa yupoyupo tu, mate yanamtoka ovyo kumbe ni dawa ya utajiri. Ajabu huyo ndiye anakuwa kipenzi cha baba ambaye anajua siri yake
Wapo ambao huambiwa kama mtoto huyo atakufa basi na utajiri nao utayeyuka, ni mambo mengi yaliyoizunguka jamii na uchafu wa tamaa za watu kutaka utajiri kwa njia ya mkato na kujikuta wakifanya uchafu au ukatili mkubwa bila kuwa na huruma ilimradi wapate utajiri.
Nayasema haya nikiwa na uchungu mkubwa baada ya baba yangu kutugeuza chuma ulete sisi wanaye kwa ajili ya kumuingizia pesa bila kujua. Nayasema haya baada ya kuteseka zaidi ya miaka saba bila kujua kumbe mateso yangu ndiyo yalikuwa chachu ya utajiri wa familia yangu.
Tangu nilipoanza kupata matatizo yaliyosababisha mateso kila kukicha, hata siku moja sikuruhusiwa kwenda hospitali zaidi ya kutumia dawa za kienyeji zilizokuwa zinapunguza maumivu na si kuniponesha.
Miaka saba nyuma, tatizo kama langu alikuwa nalo dada yangu ambaye nilimfuata mara ya nne ambaye sasa hivi ni marehemu. Mwanzo nilipomuona dada nilijua ni kidonda cha kawaida  japo kilinishangaza kuchukua muda mrefu tangu nikiwa na miaka sita mpaka nilipokuwa na utambuzi kujua kuwa dada yangu anateseka na kidonda kile ambacho kilikuwa hakiponi.
Miaka mitatu baadaye nilisikia ugomvi mkubwa kati ya baba na dada, nilijificha na kumsikia dada akisema:
“Nimechoka! Siwezi kuteseka wakati wenzangu wanafaidi kwa mateso yangu, siolewi sina maisha mazuri kama wenzangu niponipo tu. Haya maisha mpaka lini? Nasema sasa hivi naondoka na hili sasa mtafutie mwingine, nakwenda kuishi maisha yangu, kama pesa nimekuingizia sana naomba niondoke.”
“Monika mwanangu, kuondoka kwako kutaharibu kila kitu.”
“Baba acha viharibike, nimechoka.”
“Mwanangu unajua kabisa dawa hii haitaki uchafu, ukikutana na mwanaume tu umeharibu kila kitu.”
“Ndiyo maana nimekwambia tafuta wengine, baba wewe ni kiumbe gani usiye na huruma. Miaka yote nateseka peke yangu wakati wengine wanafaidi, watu wana majumba wana magari ya kifahari lakini mimi bado naishi maisha duni, kuna faida gani kuendelea kuteseka.”
“Basi nipe muda nivifanyie kazi.”
”Sina muda huo nimechoka.”
Kwa kweli kutokana na uchanga wangu wa akili, sikujua baba na dada walikuwa wanabishana nini, pia nilijiuliza dada ana mateso gani ambayo anamlalamikia baba. Lakini baada na mimi kunikuta nilielewa dada alikuwa akimaanisha nini. Maisha tuliyokuwa tukiishi yalikuwa ya ajabu sana, kwa sisi tuliokuwa tukiishi nyumbani tuliishi maisha ya dhiki sana tofauti na utajiri mkubwa tuliokuwa nao.
Tulikuwa na majumba kila kona ya Jiji la Mwanza, pia tulikuwa na mashine za kusaga na kukoboa ambazo ziliingiza pesa nyingi sana. Kaka zangu na dada zangu wote kila mmoja alikuwa na duka kubwa, gari na majumba makubwa. Lakini sisi tuliobakia maisha yetu hayakulingana na utajiri wa baba yetu.
Kitu kingine wakati ule kilichonishangaza ni hali ya mama, pamoja na kuwa na utajiri mkubwa kama ule, kila siku mama alikuwa akiamka asubuhi na kwenda shamba ambako alilima mpaka jioni na kurudi nyumbani. Kila mama aliporudi nyumbani alikuwa akirudi na kuni ambazo alipikia katika jiko la mafiga.
Kwa vile mwanzo zilikuwa akili za kitoto sikuelewa nini kinaendelea wala wakati huo sikujua faida ya utajiri tuliokuwa nao. Kitu kingine ambacho sikukielewa muda ule kilikuwa ni nyumba tuliyokuwa tukiishi. Ilikuwa ni ya zamani ambayo baba aliinunua wakati anaanza maisha.
Lakini haikuwa na mabadiliko yoyote pamoja na mabadiliko ya kimaisha kwa baba kuwa na pesa kama mchanga. Dada baada ya kubishana na baba alikaa kwa wiki mbili.
 Siku moja niliporudi sikumkuta, alikuwa ameamua kuondoka, sikujua amehamia wapi. Lakini baada ya siku tatu nilipata taarifa kuwa dada amehamia Mkuyuni ambako alikuwa amepanga na kufungua duka lake. Kuondoka kwa dada kulifanya nyumba igeuke kama pametokea msiba, kitu ambacho kilinishangaza sana.
Kuondoka kwa dada hakukuwa kitu cha ajabu kwa vile dada na kaka zangu wote walipotaka kuanza maisha yao waliondoka lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote. Baba alionekana kukosa raha, mama naye muda mwingi mkono ulikuwa shavuni. Kitu kile kwa kweli kilinishangaza sana.
                                                          ****
Nakumbuka siku moja ndugu wote walikutana nyumbani kasoro dada Monika na kuwa na kikao kizito, cha ajabu mimi nilitolewa nje hivyo kilichoendelea sikujua kwa vile nilibaguliwa kutokana na kuonekana mdogo nisiye na mchango wowote.
Baada ya kikao kilichochukua zaidi ya saa nne, ndugu zangu waliondoka.
Kuondoka kwao kidogo kulifanya baba achangamke bila kujua walikuwa wamezungumza nini na nini chanzo cha wazazi wangu kuwa katika hali ya majonzi.
 Nilijiuliza ilikuwa ni dada kuondoka au kulikuwa na jambo kubwa zaidi, katika akili yangu nilifikiria kuna umuhimu wa kumtafuta dada Monika ili nijue kwa nini ameondoka nyumbani na vilevile ni mateso gani aliyoyapata. Kuna kitu kimoja ambacho kilikuwa kikinishangaza tangu nilipopata akili. Kilikuwa ni donda la mguu la dada ambalo lilikuwepo kila siku na wala halikupata dawa ya kuliponesha.
Nilijikuta nikipata hamu ya kutaka kujua kwa nini dada aliyasema yale maneno ambayo yalionesha machungu kwa kuonekana akizuiwa nyumbani asiondoke lakini wengine wote waliruhusiwa. Kingine kilichoacha maswali kichwani mwangu ambacho kilikuwa hakijakomaa akilini ni hali ya dada kuonekana kama hajaliwi na baba tofauti na ndugu zangu tokea kwenye elimu mpaka maisha ya kawaida.
Wote walikuwa na maisha mazuri kasoro yeye, lakini sikutaka kujua zaidi kwa vile nilikuwa mtoto mdogo nisiye na uwezo wa kuhoji jambo. Nilipeleleza anapokaa dada, mama alinieleza anakaa pembeni ya Soko la Mkuyuni, duka lake linatazamana na soko. Siku moja baada ya kutoka shule nilipitia moja kwa moja hadi kwa dada.
Kufika kwake sikupotea, nilifika bila tatizo kutokana na duka lake kuonekana, pia ndilo lililokuwa  kubwa. Nilipofika dukani, dada aliponiona alifurahi sana.
“Karibu mdogo wangu.”
“Asante.”
“Umekuja na nani?”
“Peke yangu.”
“Umepajuaje hapa?” Dada alinishangaa.
“Amenielekeza mama, sehemu yenyewe si ya kupotea.”
“Ni sehemu nyeupe, karibu mdogo wangu.”
“Asante”
“Nyumbani hawajambo?”
“Hawajambo, mama anakusalimia.”
“Baba anajua umekuja huku?”
“Walaaa”
“Karibu soda upoze koo,” alisema dada huku akinifungulia soda.
Nilipokea soda na kuanza kunywa, wakati huo dada alikuwa akihudumia wateja waliokuwa wakinunua bidhaa dukani kwake, baada ya kumaliza kuwauzia alinigeukia.
“Mmh! Habari za shule?”
“Nzuri tu dada.”
“Umetumwa au?”
“Dada siji kwako mpaka nitumwe?”
“Siwajahi kukuona ndiyo maana nashangaa, ni muda gani toka niondoke nyumbani. Najua wote mlinichukia kwa kujua nataka kuwanyang’anya utajiri wenu.”
“Dada mimi sijui chochote zaidi ya baba kukukatalia na kuondoka kwa nguvu, zaidi ya hapo sijui lolote. Na mimi nikukasirikie kwa sababu gani wakati kuondoka kwako kumekuwa mateso na simanzi kwangu kama kuna uwezekano nije nikae kwako.”
“Najua mdogo wangu unanipenda, lakini baba yako hatakubali, ataona nataka kuuhamisha ukoo mzima.”
“Kwani dada kuna nini, mbona mazungumzo yako yamejaa uchungu?”
“Si wenzako wamekuja hapa bila aibu wala huruma na kuzungumza maneno ya kipuuzi,” dada alisema kwa sauti yenye kuonesha huzuni kidogo.
“Tena kweli dada kuna siku kulikuwa na kikao wote walikuwepo kasoro wewe, kwa nini hukuja?”
“Kikao hicho kilikuwa cha kunijadili mimi.”
“Wewe! Umefanya nini?”
“Unajua mdogo wangu wewe bado unakua, lakini kuna mambo ambayo sitaki yakutokee kama yaliyonitokea mimi.”
“Mambo gani?”
“Sasa hivi Masalu unazidi kukua na kupata ufahamu, kidato cha tatu ni upevuko wa akili.”
“Ni kweli dada.”
“Unajua kwa nini nimehama nyumbani?”
“Mmh, sijui.”
“Masalu sasa hivi una akili unajua zuri na baya.”
“Ni kweli dada.”
“Hivi maisha yangu ni sawa na ndugu wengine?”
“Kivipi?”
“Nina nyumba?”
“Hapana”
“Nina gari?”
“Hapana”
“Nina mtoto?”
“Unajua ni kwa nini?”
“Sijui.”
 “Hivi maisha tunayoishi ni sawasawa na utajiri wetu?”
“Hapana.”

“Hujiulizi kwa nini wengine wanafurahia maisha, wanakula chakula kizuri wanalala pazuri wanatembelea magari ya kifahari wewe na mimi tunateseka wakati baba na mama yetu ni mmoja.”
”Huwa najiuliza, nikienda kwa kina kaka au dada nakula chakula kizuri hata kulala sehemu nzuri tofauti na kwetu.”
“Hivi uwezo wa baba bado mama anaweza kulima tena kwa mkono na kuokota kuni kuja kupikia?”
“Dada hata mimi nachanganyikiwa.”
“Na wewe bila mimi kukuongeza pesa ungenunua hata chungwa ukienda shule?”
“Yaani dada toka uondoke napewa nauli ya daladala tu, tena pesa ya mwanafunzi shilingi mia.”
“Unaona sasa, hebu subiri,” dada alisema huku akimsogelea mteja kumuuzia kitu.
“Na donda lililokuwa mguuni kwangu uliliona kwa muda gani?”
“Mmh, muda mrefu sana.”
“Unaliona tena?” Dada alinionesha sehemu iliyokuwa na donda ambayo ilikuwa imepona na kuweka alama nyeusi.
“Ha! Dada umepona?”
“Nimepona mdogo wangu, lakini utajiri umeingia ufa”
“Ufa! Una maana gani?”
“Donda langu ndilo chanzo cha utajiri.”
“Unasema!” Kauli ya dada ilinishtua.
“Masalu utajiri wetu una siri nzito.”
“Siri! Siri gani hiyo?”
“Masalu utajiri wetu una siri nzito ambayo mimi ndiye niliyeibeba na sasa hivi nimeitua.”
“Una maana gani kusema hivyo?”
“Masalu kuna mambo huwezi kuyajua kutokana na umri wako, lakini kutokana na ukaribu na kuelewana kwetu sina budi kukufunulia yaliyojificha ili ujue nini kimetuzunguka. Mwanzo nisingeweza kukuambia kwa vile nimeelezwa kuwa maisha yangu hayatakuwa marefu hivyo leo nimefurahi sana kuja hapa. Haya nitakayokueleza leo si ya kutunga na kila ulilokuwa na swali nalo leo nitakupa jibu lake.
“Masalu mdogo wangu maisha yetu kabla hujazaliwa yalikuwa ya kawaida tu, baada ya baba kustaafu kazi pesa alizolipwa alinunua nyumba mnayoishi sasa hivi na pick up moja ambayo alifanyia kazi zake za kutuingizia kipato na kufungua duka ambalo lilikuwepo muda mrefu toka nikiwa darasa la nne.
“Maisha yaliendelea kama kawaida huku tukionekana familia yenye uwezo kwa sisi wote kusoma elimu nzuri. Walionitangulia wote walisoma elimu ya sekondari, lakini mimi nilipomaliza darasa la saba sikuweza kuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza.
“Lakini niliamini ningeendelea kusoma shule ya kulipia kama ndugu zangu walionitangulia. Wakati tukifanya taratibu za kunichukulia fomu ya kuanza kidato cha kwanza, siku moja nikiwa natoka chooni usiku kuna kitu kilinigonga mguuni. Nilipiga kelele kuomba msaada.
“Baba na mama walitoka na kuja nilipokuwa nimeshika mguu huku nikirukaruka, lakini ajabu hakukuonekana kitu chochote cha kuwashtua kutokana na nilivyokuwa. Nikiwa na wasiwasi labda nimegongwa na nyoka baba alinipa dawa ya maumivu na kunieleza patapoa tu.
“Usiku nililala vizuri, lakini asubuhi nilipoamka nilikuta mguu umevimba hata kutembea sikuweza. Sehemu ya juu kidogo ya mguu wa kulia kwa ndani kuliweka alama nyeusi, sikupelekwa hospitali zaidi ya kukandwa na dawa ya majani. Basi mdogo wangu mguu huo umenisumbua kwa muda mrefu bila kupelekwa hospitali.
“Hata muda wa kwenda shule ulipofika sikuweza kupelekwa shule kutokana na hali ya mguu wangu. Mpaka kipindi cha uandikishaji wanafunzi kinakwisha bado hali yangu ilikuwa tete hivyo sikuweza kujiunga na sekondari. Roho iliniuma rafiki zangu wengi walianza kidato cha kwanza. Nikawa mimi na ndani ndani na mimi, sehemu iliyokuwa na weusi ilikuwa ikiwasha na mwisho iliweka kidonda.
“Ajabu baada ya kutoka kidonda, mguu ulirudi katika hali yake ya kawaida, hata mti niliokuwa natembelea niliutupa. Niliona kama muujiza mguu wangu kurudi katika hali yake, niliamini mguu wangu ulikuwa wa kukatwa tu baada ya wazazi wangu kutoonesha juhudi zozote za kunipeleka hospitali.
“Hata nilipoweza kutembea sikuruhusiwa kutoka nje kama wenzangu, maisha yangu yalikuwa ya uani, kidonda changu kila siku kilikuwa kikivuja maji. Mdogo wangu wakati huo sikujua kama kidonda kile kilikuwa na sababu yake. Hali ya  maisha nayo ilibadilika, kulitokea mabadiliko makubwa sana.
“Kwa muda mfupi tulinunua magari, kuongeza majumba kila kona ya Jiji la Mwanza na miradi mingi, ndugu zangu walifunguliwa maduka makubwa Mwanza mjini na mimi kukabidhiwa duka la pale nyumbani ambalo liliongezwa vitu vingi. Naimani mpaka unapata ufahamu ulinikuta dada yako nina kidonda mguuni.
“Siku zote nilihoji kwa nini wazazi wangu hawataki kunipeleka hospitali au kuniwekea dawa. Baba alinieleza kuwa kama wataniwekea dawa ya aina yoyote kidonda mguu utaoza, akaniambia kitapona chenyewe, nami nilikubali mwanzo bila kujua mwisho wake utakuwa nini.
“Pia nilipewa masharti ya kutotembea na mwanaume, nikaambiwa nikifanya hivyo nitakufa. Kwa vile umri wangu ulikuwa mdogo usiotakiwa kujiingiza katika mapenzi halikunisumbua sana. Siku zilizidi kukatika huku maisha yakibadilika kila siku, nami nilivunja ungo wa kuwa na hamu ya wanaume.
“Katika wateja wangu kuna kijana mmoja ambaye kwa kweli tulipendana naye sana na kunitamkia kuwa anataka kunioa si kunichezea baada ya kumueleza simjui mwanaume. Nilimueleza mama ambaye alinikemea sana kuwa nisirudie tena kusema kitu kama kile nitaweza kukorofishana na baba.
“Kutokana na kumuogopa baba niliamua kukaa kimya, siku zilikatika huku utajiri wa baba ukizidi kuwa wa kutisha na ndugu zangu wote wakinunua magari ya kifahari na kujenga maghorofa. Kila nilipotaka na mimi kuhama nyumbani na kuanzisha duka langu, kununua gari zuri na nyumba ya kifahari kama wenzangu nilizuiwa.
“Ajabu nilikaripiwa sana tena eti nisirudie tena kusema hivyo, majibu ya mama yalinishtua sana na kujiuliza iweje wote wawe na maisha mazuri kasoro mimi? Nilijiuliza labda mimi si mtoto wa mzee Makumiyane, lakini mama alinihakikishia ni mtoto halali wa mzee Makumiyane.
“Na hilo niliamua kuliacha kutokana na kumuogopa sana baba, muda ulivyokuwa ukienda ndugu zetu wote waliondoka na kuanzisha maisha yao na kubakia sisi wawili na wazazi wetu. Roho iliniuma sana siku ndugu zangu walipokuja kututembelea, kila mmoja alikuja na gari la kifahari. Hiyo ilikuwa tisa, kumi ilikuwa harusi za ndugu zangu ambazo ziliniumiza roho na baada ya muda walipata watoto.
“Nilijikuta nikijitoa mhanga na kumfuata baba kumuomba haki yangu kama wenzangu, baba alinigombeza kama ilivyokuwa kawaida yake. Lakini nilimueleza kuwa kama hataki basi kuna siku nitatoroka na kwenda kuanzisha maisha yangu kutokana na yeye kutoonesha kunijali au kunipa haki sawa na wenzangu.
“Alinitisha kama nitajaribu kutoka nyumbani nitamtambua, vitisho vyake havikunibabaisha baada ya kuona sina faida ya kuwepo pale eti kisingizio nina duka. Siku iliyofuata nilibeba kila kilicho changu na kuondoka, mama alinibembeleza nisiondoke lakini sikubadili uamuzi wangu. Ilibidi akimbiliwe baba alipokuja alishangaa uamuzi wangu.
 “Nilimueleza nipo tayari kwa lolote atakalotaka kunifanyia, msimamo wangu ulimtisha sana baba na kuamua kuniweka chini na kunieleza siri iliyoniacha mdomo wazi.
“Nikabakia mimi siolewi, sina maisha mazuri, sina mtoto. Sikuwa na jinsi zaidi ya kuvumilia. Nakumbuka siku moja kijana ambaye alitaka kunioa alikuja na kuniulizia ombi lake, siku ile baba na mama walikuwa wamekwenda kwenye sherehe ya mtoto wa dada aliyekuwa akipata ubatizo.
“Siku ile mdogo wangu lazima niseme ukweli kwa vile sina jinsi, nilitoka na kwenda kwa yule kijana na nilifanya naye mapenzi. Kwa kweli penzi nililopata lilinichanganya nikawa sisikii wala sioni. Ilifikia wakati wa kutoroka usiku kwa kuruka ukuta na kwenda kwa yule bwana.
“Mchezo ulinichanganya sana hata kutamani kuhama nyumbani.
“Kumbe kufanya kwangu mapenzi kulikuwa kunasababisha matatizo katika familia, kwa wiki moja kulitokea mambo ya kutisha. Moja nyumba ya Malimi iliungua moto na hakuna kilichosalimika, kabla hatujatulia gari la kaka lilipata ajali mbaya iliyosababisha lisirudi tena barabarani.
“Baba naye alivamiwa na majambazi akipeleka pesa benki za mauzo ya mwezi mzima. Hali ile ilimchanganya baba na kwenda kwa mganga wake kuulizia sababu ya majanga yale. Jibu aliambiwa mali imeingia uchafu kwa mimi kufanya mapenzi.
“Baba alikuja juu na kunitishia, nami sikumuogopa nilimueleza ukweli kama mimi ndiye chanzo cha utajiri kwa nini niwe na maisha duni wakati watu wasiojua adha niipatayo kutokana na mali wanazochezea kuishi maisha mazuri. Nilimueleza baba kuwa kama hatanipa mali tena iwe zaidi ya ndugu zangu wote lazima nitaondoka na kwenda kuishi maisha yangu.
“Baba alinitisha kwa kusema kama nitaondoka sitakaa muda mrefu lazima nitakufa, vitisho vile sikuviogopa na kumhakikishia kuwa nitaendelea na msimamo wangu na nipo tayari kufa lakini si kuwa kitega uchumi cha watu. Mama naye aliingia kwenye kazi ya kunibembeleza ili nibadili tabia zangu zilizoonekana chafu.
“Nilikubali kubaki nyumbani kwa masharti na mimi natakiwa niwe na gari na duka kubwa ambalo nitalimiliki mwenyewe. Tulikubaliana na mimi kufuta wazo la kuondoka nyumbani. Nilisubiri kutekelezewa niliyoyataka kwa hamu kubwa, nami nilikuwa na hamu ya kuendesha gari, nilikuwa na hamu ya kumiliki mali yangu mwenyewe.
“Siku zilikatika bila kuona dalili zozote za kununuliwa gari wala nyumba, wakati huo nilikuwa nimesimamisha mapenzi na shemeji yako. Mambo yalizidi kunyooka kwa  Malimi aliyeunguliwa nyumba yake kujenga ghorofa analoishi sasa.
“Lakini mwenyewe sikuona kitu chochote, kila nilipouliza niliambiwa nisubiri mambo hayajakaa vizuri. Mambo hayajakaa vizuri wakati ndugu zangu kila kukicha  walibadilika kimaisha? Niliona kama wananichezea, nikaanza kuweka pesa zangu taratibu bila kumshirikisha mtu.
“Shemeji yako nilimtuma anitafutie sehemu ya kufungulia duka akapata huku, nilimpa pesa za kulipia mwaka mzima na kumuagiza anunue vitu vyote muhimu kwa ajili ya duka naye alifanya kama nilivyomuagiza. Unajua Masalu katika maisha yangu huwezi kuamini toka nipatwe na tatizo la mguu lililozaa kidonda sikuruhusiwa kwenda kanisani.
“Ndugu zangu wote ndiyo waliokuwa wakienda kanisani, lakini mimi nilizuiwa kwa kuambiwa kama nitakwenda kanisani nitasababisha maafa makubwa kuliko yale ya kutembea na mwanaume. Nilijiuliza mimi ndiye sitakiwi kwenda kanisani lakini wadogo na dada zangu wote mlikuwa mnakwenda, kwa nini?
“Nilikatazwa hata kusoma Biblia, baba alisema mizimu haitaki kuchanganya mambo ya Mungu na mizimu. Basi nilibakia simjui Mungu wala kanisa. Baada ya kukamilisha vitu vyote muhimu vya dukani, shemeji yako alilisifia duka alivyolijaza. Nilijipanga kwa siri na siku moja nilitoroka usiku na nguo zangu bila wao kujua. Masalu siku mlipoamka na kunikosa ilikuwaje nyumbani?” Dada Monika aliniuliza huku akiwa ametuliza macho usoni kwangu.
“Mmh, kwa kweli walichanganyikiwa sana, walihaha kila kona, familia yote iliitwa asubuhi ile na kukutana. Hata mimi nilizuiwa kwenda shule, kilikuwa kikao kizito kilichokujadili. Niliwasikia wakisema bila kukuona kila kitu kitaharibika, siku ile hakuna kazi iliyofanyika, maduka yote yalifungwa na kuanza kukutafuta.”
“Basi mdogo wangu nilikuja huku kuanza maisha yangu ili kupata uhuru wa maisha wa kupanga mambo yangu bila kuingiliwa na mtu. Pesa niliyokusanya niliamini mpaka iishe nitakuwa nimepiga hatua kubwa katika biashara kwa vile nilikuwa naijua vizuri.
“Walianza upelelezi wa chinichini na kumjua mpenzi wangu ambaye walimbana kwa kumpeleka polisi ili awajulishe nilipo. Mwanzo aligoma kutokana na masharti niliyompa kama wazazi wangu watamuona asikubali. Mpango wetu ulikuwa kuishi pamoja nami nilitaka yeye asirudi tena kule.
“Lakini kwa vile familia yake ipo kule walifanikiwa kumpata na baada ya kumbana sana aliwaleta hapa. Kama utakumbuka siku waliyokusanyana kuja kwangu ilikuwa baada ya kumtuma mtu kwa siri bila kujua ninapofanyia kazi zangu na kuamua kukusanyana kuja hapa ili nikubali kurudi nyumbani.
“Basi walipofika kila mmoja ooh, Monika umefanya vibaya kuondoka nyumbani wakati unafahamu kila kitu. Niliwaeleza siwezi kuumia mimi wakati wenyewe wanakula maisha, kama hivyo basi kidonda changu achukue mtu mwingine. Hakuna aliyekuwa tayari kuchukua ugonjwa wangu.
“Nilijua mkuki kwa nguruwe ila kwa binadamu mchungu, mwisho wa yote walikubali niendelee na kazi zangu kwa makubaliano nisitembee na mwanaume au kukitibu kidonda. Niliwakubalia ili kuwaridhisha kuwa nitafanya kama wanavyotaka. Lakini sikuwa tayari kukubaliana na ujinga wao tena.
“Nami nilikuwa na hamu ya kuwa na mwanaume ambaye muda ule alikuwa akija mara moja na wakati huo ndiyo alikubali kuhamia kwangu kabisa.
“Baada ya kuondoka niliendelea na mpenzi wangu ambaye muda huo nilikuwa nakaa naye nyumba moja, kupika na kupakua, sasa hivi yupo kwenye mihangaiko yake muda wake wa kurudi ni saa moja usiku. Ila jumapili huwa haendi popote.
“Tangu nihamie huku siku hizi nakwenda kanisani kama kawaida, ajabu ya Mungu kidonda kilianza kupona chenyewe bila kukiwekea dawa. Kumbe kidonda changu kilivyokuwa kikipona na mambo yalibadilika katika utajiri wa familia yetu. Matatizo yalitawala kwa maduka kuibiwa vitu vyote bila kujua tatizo ni nini.
“Kama kawaida walirudi kwa mganga na kuelezwa kuwa nimeishapona pia ninaendeleza kufanya uchafu katika mali ya familia yangu. Walijikusanya kama ilivyo kawaida na kuja kuniomba niokoe mali ya familia, niliwaeleza katu sitakubali kufanya tena ujinga ule.
“Baada ya juhudi zote kushindikana baba aliniapia mwaka huu siumalizi lazima nitakufa. Nilimhakikishia yeye si Mungu, kama kufa nitakufa kwa amri ya Mungu. Wote waliondoka vichwa chini wakiamini wanarudi katika maisha ya kawaida, tokea siku hiyo sijawaona tena na maisha yangu  yanaendelea kama kawaida na muda si mrefu nawe utapata mjomba.”
“Dada una mimba?”
“Ndiyo mdogo wangu.”
“Mmh, Mungu mkubwa.”
“Basi mdogo wangu siri uliyokuwa huijui ndiyo hiyo, nasikia sasa havi mambo yote hayaendi vizuri kabisa na wamechanganyikiwa.”
“Ni kweli dada sasa hivi kila siku baba analalamika na kusema angekuwa na uwezo angekuulia mbali.”
“Sasa aniue kwa sababu gani? Kwa watoto wa mzee Makumiyane ni mimi peke yangu? Niliwaeleza mmoja ajitoe akichukue kidonda change lakini kila mmoja alikaa nyuma kukikimbia kidonda. Basi mdogo wangu nikifa leo ujue nimekufa kwa kukikataa kidonda.
3
“Siogopi kufa hata siku moja, kila kiumbe kitakufa! Kama nitakufa kwa kukataa kidonda nipo tayari, ila namuomba Mungu aniue baada ya kumzaa mwanangu ili niache jina langu,” dada alisema huku machozi yakimtoka,  moyo wangu uliingia baridi ya woga wa ajabu kwa yote niliyoelezwa na dada juu ya siri nzito ya utajiri wetu iliyokuwa ikibebwa na kidonda cha dada.
Kingine kilichonitisha kilikuwa kusikia kuwa dada eti atakufa baada ya kukikataa kidonda. Machozi ya dada yaliniumiza sana moyo wangu na kumuonea huruma.
“Dada kwa nini usikubali kuliko kukubali kufa?”
“Masalu wewe hujui lolote katika maisha, lakini unakumbuka haya niyasemayo  hata kama nikifa leo utayakumbuka maneno yangu. Kwa vile wote wameshazaa na kufanya mapenzi hawawezi kupatwa na kidonda. Wasiwasi wangu kikitoka kwangu kinaweza kurudi kwako.”
“Ha! Dada mbona unanitisha.”
“Kutokana na siri ya kidonda niliyoelezewa na baba, nakumbuka nilimuuliza kwa mfano nikifa itakuwaje? Alinieleza itabidi atafutwe aliye safi ndani ya familia. Nilimuuliza tena ni kwa mwanamke tu? Alinijibu ni kwa mtu yoyote mwanamke au mwanaume aliye msafi, unafikiri nani atakayekichukua kidonda changu kama si wewe?”
“Mimi sikubali.”
“Masalu huna jeuri ya kumbishia baba.”
“Nitahamia kwako.”
“Uhamie wapi nami umesikia lazima nitakufa?”
“Huwezi kufa dada, ni vitisho.”
“Hata nisipokufa siwezi kukukubali tena hicho kidonda kisicho na faida zaidi ya mateso.”
                                                                     ****
Kwa kweli sikuweza kumshawishi dada kutokana na msimamo wake mkali, jioni ilipofika niliagana na dada kwa kupanda daladala mpaka nyumbani. Nilipofika nyumbani nilikuwa na mawazo mengi juu ya maneno ya dada ambayo sikuamini kama yana ukweli wowote, nilipinga kuwa utajiri wetu si kupitia kidonda chake. Nilipoangalia hali ya maisha yetu ilikuwa ya kawaida tofauti na kauli ya dada ya kusema sasa hivi maisha ni magumu upande wa familia.
Chakula tulikula kama kawaida ambacho kwa kweli hakikuwa na hadhi ya utajiri uliotuzunguka. Lakini kwa muda ule sikushtuka kutokana maisha yale ndiyo yaliyokuwa ya kawaida ya siku zote. Japo kwa mbali nilijawa na maswali iweje nyumbani maisha yetu ya kawaida.
Kingine ambacho alikisema dada kiliniingia akilini kilikuwa kwa mama kuamka kila siku asubuhi na kwenda kulima wakati baba alikuwa na pesa nyingi. Kingine nilichokubaliana na dada ni mama kuokota kuni na kuja kupikia wakati dada zetu wanatumia majiko ya umeme na gesi.
Lakini kitu ambacho sikukubaliana naye ni imani za kishirikina kwanza maisha yetu yanategemea ushirikina wa kidonda chake. Katika akili yangu niliamini kidonda cha dada hakikuwa kimepata tiba sahihi. Lakini baada ya kupata tiba sahihi kilipona.  Niliamini dada alitaka kunijengea uadui na wazazi ili niwaone ni watu wabaya wasiofaa.
Sikutaka kumuamini dada zaidi ya kuona anataka kunipotosha, lakini siri ile nilibaki nayo moyoni sikutaka kumwambia mtu. Siku zilizidi kukatika nami niliendelea na masomo kama kawaida. Pamoja na kuyapuuza ya dada na kuyaona kama ya uchonganishi lakini kuna vitu vilikuwa vikitia wasiwasi. Kuna siku nilimsikia baba akimwambia mama kwa sauti iliyoonesha hawakuniona kutokana na kiza kilichokuwepo.
“Mama Monika nimempa mpa muda mwanao wa kutosha, litakalotokea tusilaumiane.”
“Sasa mimi nitafanyaje kama mwenyewe hajihurumii.”
“Hali ni mbaya tukiendeleza huruma tutaadhirika.”
“Baba Monika mimi mwenyewe nilikwenda kwa Monika, lakini kiburi kimemjaa tena amekosa hata heshima kujua anazungumza na mama yake.”
“Mganga amenipa mwezi huu mwisho la sivyo kihame kwa mwingine.”
“Unafikiri kitaenda kwa nani?”
“Hilo suala tutalizungumza baada ya kushindikana kabisa.”
“Yaani Monika kanichanganya sana.”
“Basi uamuzi ni huo sina mwingine.”
“Utakavyokuwa mimi tena simo kayataka mwenyewe.”
Mazungumzo ya baba na mama kumhusu dada Monika yalinishtua sana na kujiuliza baba alikuwa anataka kufanya nini? Nilijiuliza au ndiyo niliyoelezwa na dada Monika juu ya kumlazimisha aendelee kuwa na kidonda na kama kikihama kitaenda kwa nani?”
Pia nilijiuliza mama alikuwa na maana gani kusema yakimkuta dada Monika hayumo ni mambo gani hayo. Nilijikuta nikiingiwa na wasiwasi wa maneno ya dada Monika kuwa baba alimtishia maisha kuwa kama akikataa kuendelea kuwa na kidonda hatadumu lazima atakufa.
Nilijikuta nikikosa raha na kutamani kwenda kumuomba dada akubali kuliko kutokewa na balaa lile. Kwa mbali nilijikuta njia panda kuamini kuwa kidonda cha dada ndicho kilikuwa kikifanya tuwe matajiri. Nilitamani nizungumze na mama kuhusu kujua baba alikusudia kufanya nini kwa dada.
Japo niliogopa kuulizwa nimejuaje, lakini nilipanga siku ya pili sitakwenda shule na kumfuata mama shambani kumuuliza kuna kitu gani dada Monika anataka kufanyiwa baada ya kukataa kuwa na kidonda kile. Usiku kwangu ulikuwa mzito sana niliota mambo mazito ambayo yalinitisha na kunifanya niamke saa nane za usiku na kukesha bila kulala.
Niliota familia yetu ikifanya sherehe kubwa huku dada Monika akiwa amekufa na mwili wake haukuwa na mguu mmoja uliokuwa ukivuja damu, ule mguu uliokuwa na kidonda. Damu ya dada Monika ndugu zetu walikuwa wakinywa kwa furaha. Niliamka na kukaa kitandani nikitweta. Nilijiuliza ndoto ile ina maana gani.
Baada ya muda usingizi ulinipitia, muda haukupita niliota ndoto nyingine mbaya, niliota nimeoza mguu sehemu ya ndani na kuanza kutoka funza, ajabu ndugu zangu walifurahia kama ndoto ya mwanzo ya kufurahia kifo cha dada Monika kwa kumla na kunywa damu yake.
                                                            *****
Nilishituka usingizini na kuogopa kulala tena mpaka asubuhi, asubuhi nilisingizia naumwa. Sikwenda shule, nilitoka ndani na kwenda kulala sebuleni ili kuogopa kuota ndoto za kutisha. Sebuleni nilipolala sikuota ndoto mpaka nilipoamka kujiandaa kwenda kwa mama shamba baada ya kufungua kinywa.
Nilioga na kufungua kinywa kisha nilielekea shambani kwa mama ili nikamuulize kuna kitu gani dada Monika anataka kufanyiwa na baba, kama kumuua ningepinga kwa nguvu zangu zote.
Nilikwenda hadi shambani na kumkuta mama akiwa katikati ya kilimo, sikumsemesha kitu, nilijiuliza iweje tuwe na pesa majumba na magari mama ateseke kiasi kile. Nilizidi kuingiwa na wasiwasi juu la mambo yaliyokuwa yakifanyika.
Baada ya muda nilimwita mama, aliponiona alishtuka na kuniuliza.
“Masalu kuna usalama?”
“Upo mama.”
“Si unaumwa, umekuja huku kufanya nini?”
”Kuna kitu nataka kuuliza mama.”
“Kitu gani?”
Mama alisema huku akiweka pembeni jembe na kunifuata nilipokuwa nimesimama.
“Masalu una nini mwanangu?”
“Mama jana nimeota ndoto mbaya sana.”
“Ndoto gani mwanangu?”
“Kuhusu dada Monika.”
“Monika! Ndoto inahusu nini?”
Nilimhadithia ndoto niliyoota, mama alishtuka na kutulia kwa muda kisha alisema kwa sauti ya chini.
“Sasa wewe wasiwasi wako nini?”
“Mama kuna maneno nilizungumza siku moja na dada Monika kuhusu baba kumtishia kifo na kunieleza kama akifa nijue baba ndiye aliyehusika.”
“Masalu!” Mama alishtuka.
“Naam mama.”
“Mlifikia wapi mpaka mkazungumza hayo?”
“Kuna siku nilikwenda kwa dada Monika na kumuuliza sababu ya yeye kuhama nyumbani. Mama dada alinieleza mambo mengi ya kutisha sana lakini sikuyaamini.”
“Masalu alikueleza mambo gani Monika?”
Nilimuhadithia baadhi ya mambo kisha nilimueleza ya yeye kulima wakati tuna pesa.
“Eti mama hata kulima kwako amesema ni imani za kishirikina iweje tuwe na pesa wewe ulime wakati ungewalipa watu wakatulimia?”
“Mmh, mbona makubwa!” Mama alizidi kushangaa.
Mama alisema huku akitoka shambani na kunisogeza chini ya mwembe.
“Masalu wewe hayo unayaamini?”
“Siwezi kuyaamini japo kuna mengine yana ukweli.”
“Nakuomba asikubaliane na maneno ya Monika ni ya uongo.”
“Mama mbona baba alisema jana litakalomtokea asilaumiwe, nini kitamtokea dada Monika?”
“Wee Masalu!” Mama alizidi kushtuka kuona ninajua vitu vingi.
Ilionesha mama aliamini siyajui mengi kuhusiana na mambo yaliyokuwa yakitendeka nyumbani. Nilimuona akifuta jasho kwenye paji la uso kisha alinipandisha na kunishusha na kusema.
“Masalu wewe ni mtoto, hujui kitu hata nikikueleza hutanielewa, nakuomba uachane na hayo, swali hili ungemuuliza baba yako mngekosana.”
“Mama hujanijibu, jibu si kukosana bali kupata ukweli nilioelezwa na dada Monika juu ya kukataa kwake kidonda na baba kumtishia kuyakatisha maisha yake.”
“Hilo si kweli, ni ujinga wa dada yako kama kufa atakufa na yake.”
“Mama, baba aliposema kuwa asilaumiwe na wewe kusema shauri yake alikuwa na maana gani?”
“Masalu naomba usiniulize swali kama hilo tena,” mama alikuwa mkali.
Niliona nibadili mada kwa kumuuliza swali lingine.
“Halafu mama kwa nini tusitafute mtu atulimie na wewe kupumzika, tuna faida gani kuwa na pesa na wewe mama unaendelea kuteseka?”
“Masalu nakuomba uondoke, nakuona umekosa maneno ya kuzungumza,” mama alikuwa mkali.
Kila neno nililolisema kwa mama lilimuudhi, sikutaka kuendelea kulumbana naye, niliamua kurudi zangu nyumbani nikiwa bado nipo njia panda. Wazo la haraka lilikuwa kwenda kwa dada Monika kumueleza akubaliane na matakwa ya wazazi ili asije kujutia maisha yake. Nilipofika nyumbani nilijawa na mawazo mengi sana kuhusiana na majibu ya mama.
                                                            *****                                                     
Nilipanga siku ya pili nitaaga na kwenda shule lakini kituo changu cha kwanza kingekuwa kwa dada Monika kumueleza hali halisi kutokana maneno ya baba. Siku ile sikushinda na furaha kila nilipokumbuka ndoto nilizoota usiku na majibu ya mama.
Japo niliamini mama hawezi kumueleza baba niliyomuuliza, bado nilikuwa na wasiwasi kama atamueleza basi lazima baba angenishikisha adabu kufuatilia mambo yasiyonihusu. Lakini siku ilikatika bila kuulizwa swali lolote na baba zaidi ya mama kuniita na kunionya nisirudie tena kuuliza mambo yale wala kumueleza mtu yoyote.
Nilimuahidi mama sitarudia kumueleza mtu maneno yale, kwa furaha ya mama alinipa pesa za kula shule kitu ambacho hakuwahi kukifanya zaidi ya kila siku kunipa nauli tu. Niliamini ile itanisaidia kuongeza nauli ya kwenda kwa dada. Usiku nilipolala ndoto ya jana yake ilijirudia.
Nilijikuta nikikesha kwa mara nyingine mpaka asubuhi kwa kuogopa kila nilipofumba macho njozi mbaya zilinifuata. Chumba nilikiogopa na kujiuliza njozi zile mbaya za dada Monika kuliwa nyama huku familia yote ikifurahia zilikuwa na maana gani? Kingine kilichonitisha mguu wangu kuoza na kutoa wadudu.
Nilijikuta nikiogopa kufumba macho na kubaki macho mpaka kunakucha, alfajiri nilisikia habari zilizonishtua sana. Nilimsikia baba akimwambia mama:
“Aliyoyataka mwanao yametimia.”
“Unataka kuniambia Monika ame...”
“Ishia hapohapo na sitaki utoe chozi unajua nini tuliambiwa.”
Nilishtuka na kutoka nje na kuwakuta baba na mama sebuleni, mama aliponiona alishtuka tofauti na baba.
“Mama dada Monika kafanya nini?”
“Kwani umesikia nini?” Baba aliniuliza.
“Sijui...ame..”
“Amefanya nini?”
“A..me..mee,” nilijikuta nikipata kigugumizi.
“Hebu ondoka hapa asubuhi yote nini kimekuamsha,” baba alinifokea.
Nilirudi chumbani kwangu nikiwa bado sielewi dada Monika kafanya nini japo bado wasiwasi wangu ulikuwa labda amefariki kutokana na maelezo ya dada Monika na kauli ya baba juu ya dada Monika. Kwa kauli ya baba ambayo aliifunga, niliamini kabisa dada Monika huenda kweli amefariki. Kwa vile muda wa kujiandaa kwenda shule ulikuwa umekaribia nilikwenda kuoga ili nijiandae na shule.
Baada ya kuoga nilirudi chumbani kwangu kujiandaa kwenda shule, nikiwa bado nipo katika maandalizi nilishtuka kusikia sauti za ndugu zangu, ujio wao wa asubuhi ile ulinishtua sana.Niijiuliza kuna kitu gani kimetokea au ndiyo niliyokuwa nayafikiria ya kifo cha dada Monika? Sikutaka kutoka haraka, nilimalizia kuvaa nguo za shule, baada ya kuvaa nilitoka ili nijiandae.                                                             
Nilishtuka kuwaona dada na kaka zangu wamekaa sebuleni, waliponiona walishtuka na kuniuliza:
“Masalu unakwenda wapi?”
”Shule.”
“Unakwenda shule hujui hapa nyumbani kumetokea nini?”
”Sijui.”
“Mmh, makubwa, Monika amefariki.”
“Eti?
“Monika amefariki.”
“Dada Monika?” Bado sikuamini.
“Eeeh, huyo huyo.”
“Siamini …siamini.”
Bila kujielewa nilijizoa mzimamzima na kujipiga chini na kupoteza fahamu, baada ya huduma ya kwanza nilipata fahamu na kuangua kilio tofauti na wenzangu ambao hakuna hata mtu mmoja aliyemwaga chozi. Juhudi za kunibembeleza zilishindikana. Bila kujielewa nilijikuta nikisema kwa sauti ya juu:
“Yote uliyonieleza dada yangu nilifikiri utani kumbe kweli wamekuua.”
“Alikueleza nini?”
”Baba kwa nini umemuua dada Monika?”
“Wee Msalu maneno gani hayo?”
“Maskini dada yangu kumbe ulikuwa na siri nzito moyoni mwako ambayo imenifumbua leo, ungekufa dada yangu bila kujua lakini Mungu mkubwa.”
“Masalu hebu ondoa uchuro hapa.”
“Siwezi… siwezi, kwa nini lakini umemuua dada Monika?” Niliendelea kulia kwa uchungu huku nikijipigiza chini.
“Nani kamuua Monika?”
“Nyinyi wote kwa tamaa za mali.”
“Masalu unatukosea adabu.”
“Siwakosei adabu bali ukweli ni huo.”
Kaka mkubwa alinichukua na kutoka na mimi uani huku nikiendelea kulia, roho iliniuma kumpoteza kipenzi dada yangu Monika mtu aliyenipenda kuliko yeyote. Kutokuonesha ndugu zangu kuguswa na kifo cha Monika niliamini ndoto niliyoota ilikuwa na maana kubwa. Kama dada Monika wamemla nyama nini maana ya kidonda mguuni kwangu chenye kutoa wadudu?
                                                        ****
Tulipofika nje kaka alinibembeleza na kunieleza maneno ya busara kuhusiana na kifo cha Monika kuwa kilitokana na uzazi wala hakihusiani na masuala ya ushirikina. Na kutokuonesha kuguswa kila mmoja alikuwa akililia moyoni kwa vile hakuna aliyetegemea.
Kwa vile nilikuwa namheshimu nilimkubalia ili kumridhisha lakini siri ilibakia moyoni mwangu. Wengi walishtuka maneno yangu na kunionya nisiyasikilize ya Monika kwa vile alikuwa ni muongo na mgombanishi, nao nilikubaliana nao ili yaishe.
Ajabu ya mwaka ambayo baada ya akili ya ufahamu kukomaa niligundua kuna kitu kilitendeka mpaka leo hii sijui. Baada ya taarifa za msiba wa dada Monika ambao  hakuna aliyefunua mdomo wake kulia zaidi  yangu mwenyewe.
Taarifa za msiba ule hata majirani hawakujua nyumbani kulitokea msiba. Mwili wa dada ulifuatwa na kurudishwa nyumbani. Gari lililouleta mwili wa dada ilipita mpaka uani. Waliuteremsha na kuuingiza chumbani kisha ndugu wote walitawanyika kwenda kuendelea na kazi zao kama kawaida. Kitu kile kilinishtua iweje kuwepo na msiba hakuna mtu aliyeguswa wala taarifa kuwafikia majirani.
Usiku nilipelekwa kwa kaka ambako nililala siku mbili na kurudishwa nyumbani, niliporudi hali ilikuwa ileile na kunifanya niwe na mawazo ni kweli dada alikufa au taarifa zile zilikuwa mgonjwa mahututi? Kwa hiyo yupo hospitali, sikutaka kuhoji haraka baada ya wiki sikuona mabadiliko wala taarifa zozote za dada Monika.
Hata majirani waliotuzunguka hawakujua kitu zaidi ya ndugu wa mpenzi wa dada Monika kuulizia dada alizikwa wapi. Maswali yale kwa kweli yalinichanganya sana. Kila nilivyojitahidi kuchunguza sikupata taarifa zozote zaidi ya watu kufurahia maisha.
Mwezi ulikatika nikiwa bado njia panda kuhusu maswali dada Monika wakiulizia mazishi yake yalifanyika lini na kwa nini baba hakuwataarifu kama kuna msiba, kama majirani wajumuike pamoja katika msiba ule. Siku moja nilikwenda hadi Mkuyuni kwenye nyumba aliyokuwa akikaa dada Monika.
Nilikuta mlango umefungwa, kuuliza nilishindwa kutokana na kuogopa maswali huenda amekufa na kunifahamu mimi ni nani. Niliamua kurudi bila kupata jibu kuhusiana na kupotea kwa dada Monika kwamba amekufa kweli au hali yake ni mbaya. Lakini nilikumbuka kaka mkubwa aliniambia kuwa Monika alikufa kutokana na uzazi.
Nilijiuliza kama alikufa alizikwa wapi na kwa nini majirani hawajui lolote, na kama kweli alikuwa amekufa mazishi yake yalifanyika wapi. Kutokana na kuja mjini muda mrefu mazishi yote tuliyafanyia mjini. Ingekuwa kama wengine mazishi huyafanyia vijiji walikozaliwa lakini dhana ile baba aliikataa.
Bado sikutaka kukubali, nilizunguka kwenye makaburi labda nitaliona kaburi jipya la dada Monika, lakini sikuona kitu chochote zaidi ya makaburi mapya yenye majina tofauti na la dada Monika.  Nilibakia njia panda siku zote kujiuliza ni kweli dada Monika alikufa au yupo kwa mganga.
Siku moja nilikutana na shemeji aliyekuwa akikaa na dada Monika, nilimuulizia kitu ambacho kilionekana kituko mbele yake.
“Shemu za siku?”
“Nzuri sijui zako?”
“Eti shemu dada Monika yupo wapi?”
“Masalu swali gani hilo? Ina maana mtu akifa huwa anakwenda wapi?”
“Una maana ni kweli dada Monika amekufa?”
“Masalu kioja gani unataka kunionesha, ina maana wakati Monika anakufa wewe ulikuwa wapi?”
“Sasa kama amekufa maiti yake imezikwa wapi?”
“Mimi nitajua wapi, wakati nilifukuzwa?”
“Kama kazikwa mbona hakuna kaburi lake?”
“Masalu upo sawa?”
“Kwani wewe unanionaje?”
“Nakuona haupo sawa.”
“Nipo sawa na akili timamu.”
“Kama kweli una akili timamu usingeniuliza suala la kifo cha Monika.”
“Shemu kama dada alikufa mbona wewe mumewe haukuwepo msibani?”
“Masalu, nilifukuzwa kama mbwa na kutishiwa maisha, kwanza nikionekana nimesimama na wewe nitajitafutia balaa.”
“Shemu una uhakika Monika amekufa?”
“Ndiyo.”
“Ulimshuhudia kabisa amekufa?”
“Monika amefia mikononi mwangu na kuna mengi alinieleza ya kukueleza lakini sikupata muda wa kuonana na wewe. Kama ni kweli aliyosema Monika basi familia yetu itakuwa ina hatari kubwa.”
“Kuhusu utajiri?” Nijikuta naropoka.
“Nalo hilo alilizungumzia, ila wamemtesa sana mke wangu mpaka kifo chake. Kibaya wamemuua hata mtoto wangu aliyekuwa tumboni bila kosa, yaani siamini familia yako kuna na roho mbaya kiasi hicho. Kama mtu kawapatia utajiri akisema amechoka na yeye anataka maisha yake kuna ubaya gani?” Maskini shemeji yangu alizungumza huku akitokwa na machozi, nilijikuta nikitokwa na mimi machozi bila kupenda.
“Masalu familia yenu haifai, unafikiri maisha ya kuongozwa na nguvu za kishirikina mwisho wake nini? Haya sasa wamemuua Monika nani atafuata na kwa taarifa kidonda alichokikataa dada yako kitahamia kwako. Kabla ya kufa kaitaja familia yenu wote kuwa wanagombania roho yake kasoro wewe pake yako na kuonesha jinsi gani huhusiki na mateso ya mke wangu.”
“Mungu wangu!”
“Huo ndio ukweli wenyewe, hujiulizi kwa nini mama yako bado analima kama sio ushirikina, hivi baba yako hana pesa ya kuwapa watu walime na mama yako na utu uzima wake apumzike?”
“Anaweza.”
“Kama anaongeza majumba na magari kwa nini mama yako usipumzike, hebu angalia ndugu zako wakubwa. Nao wana roho ya tamaa ya mali kushindwa kumuonea huruma mama yenu. Nasikia ndani mwenu kuna chumba kisichofunguliwa, unajua kuna nini?”
“Hata sijui!”
“Kwa taarifa yako kuna maiti ya mtoto mchanga ambayo kila baada ya siku tatu hupakwa mafuta ili isiharibike.”
“Shemuuuu! Umejuaje?” Nilishtuka kusikia habari zile, chumba alichokisema kweli kilikuwepo ambacho sikuwahi kukiona kikifunguliwa.
“Dada yako Monika alikuwa na siri nzito moyoni mwake, nyingine alisema hawezi kuniambia labda ungekuwepo kabla ya kufa kwake.”
“Sasa yeye alijuaje kama kuna maiti ya mtoto?”
“Mara nyingi kazi ile aliifanya yeye, baba na mama yenu. Hakuna mtu mwingine aliyeruhusiwa kuifanya.”
“Mmh! Maiti ya mtoto wa nani?”
“Kama una kumbukumbu, nasikia mtoto wa kwanza wa dada yako ambaye ndiye aliye na pesa kuliko wote alimtoa mtoto wake kafara ili kuongeza utajiri.”
                                                                    *****
Kauli ile ilinirudisha nyuma na kukumbuka miaka sita iliyopita dada mkubwa alifiwa na mwanaye lakini mazishi yake sikuyaelewa japo msiba ulikuwa nyumbani. Kingine kilichonifungua macho hakikuwa na tofauti na msiba wa Monika kilikuwa cha kifamilia tena ya ndani hata wanandugu hawakujulishwa. Taratibu nilianza kufunguka akili na kuamini kila lililosemwa na Monika lilikuwa na ukweli mkubwa.
“Asante shemu kwa kunifumbua macho,” nilimshukuru ili tuagane, nilipotaka kuondoka aliniuliza kitu.
“Masalu unataka kuniambia hukuwa na habari Monika amekufa au ulitaka kunitega akili?”
“Shemu, huwezi kuamini kila dakika nimekuwa nikichanganyikiwa juu ya taarifa za msiba wa dada Monika. Kweli niliuona mwili ukiteremshwa kwenye gari. Lakini tokea hapo sikuweza kujua nini kilichoendelea mpaka leo hii.”
“Ulipouliza walikujibu nini?”
“Sijauliza bali nilifanya upelelezi wangu, kila kona nilifika lakini sikupata kuona chochote.”
“Ulichunguza nini?”
“Sehemu za makaburi au kupata taarifa kama hajafa yupo wapi?”
“Una uhakika Monika hakuzikwa?”
“Nina uhakika.”
4
“Basi kuna sehemu wamemuweka, isiwe naye wamemuweka kwenye hicho chumba  na kumpaka mafuta?”
“Mmh! Sijui.”
“Unaweza kuingia?”
“Mmh! Nitajitahidi kuhakikisha napata ukweli.”
“Basi utakachokipata usikose kunijulisha.”
“Nakuahidi kukuletea kila kitu.”
“Haya shemu kwaheri.”
“Ya kuonana.”
Niliagana na shemu na kurudi zangu nyumbani, nilizidi kuchanganyikiwa na maneno ya pande mbili juu ya ukweli juu ya kifo cha dada Monika. Moyoni niliapa nikipata muda lazima mama ataniambia ukweli.
Siku zilikatika bila kujua taarifa za uhakika kuhusiana na habari tata juu ya kifo cha dada Monika ni kweli amekufa? Kitu ambacho moyo wangu haukukubaliana nacho. Uvumilivu ulinishinda, siku moja nilimfuata mama shambani kutaka kujua ukweli wa dada Monika. Kama kawaida yangu nilidanganya naumwa.                                                        
*****
Baada ya kuondoka na kuniacha nyumbani na mfanyakazi, majira saa nne asubuhi nilikwenda hadi shamba. Nilimkuta mama akipiga jembe kama hana akili nzuri. Moyoni nilimuonea huruma jinsi alivyohenyeka japo tuna pesa, kila dakika niliyakumbuka maneno ya dada Monika kuwa maisha yetu yanaongozwa na ushirikina.
Nilimwita mama ambaye alishtuka kuniona, niliamini kabisa alijiandaa kutokana na kumuuliza maswali mazito siku ya kwanza.
“Wee Masalu mbona huku si unaumwa?”
“Kidogo nimepata nafuu.”
“Haya ulikuwa unasemaje?”
“Kuna kitu mama kinanisumbua kila siku naomba msaada wako kwani naweza kuwa chizi.”
“Wee mwana mbona una mambo kuna nini tena?”
Mama alisema huku akiweka jembe pembeni na kunifuata nilipokuwa nimesimama.
“Masalu  kuna  nini tena?” Mama aliniuliza huku akifuta jasho kwenye paji la uso kwa mkono.
“Mama toka kifo cha dada Monika kuna mambo yamekuwa yakinichanganya na kunifanya kila siku nisijielewe.”
“Masalu mambo gani tena mwanangu kila siku huishi vioja?”
“Kuhusu dada Monika.”
“Monika kafanya nini tena?”
“Mama ni kweli dada Monika amefariki?”
”Masalu wewe si mtoto mdogo sasa, kila mtu anajua Monika amefariki wewe ukiwemo.”
“Mamaa, kama dada Monika amefariki mbona sikuona mazishi wala kaburi lake.”
“Masalu uyaone hayo ili yakusaidie nini?”
“Mama unajua majirani wanatusema vibaya toka taarifa za kifo cha dada Monika.”
“Nani aliwaambia Monika amekufa?”
“Mamaa, kwani kifo cha dada Monika kilikuwa cha siri?”
“Hata kama sio cha siri sio lazima wajue.”
“Hivi mama watu wakiniuliza dada Monika yupo wapi mimi niwajibu nini?”
“Wanyamazie usiwajibu chochote.”
“Lakini mama, kumbe hata yule shemeji aliyekuwa anakaa na dada Monika mlimfukuza asihudhurie mazishi?”
“Ahudhurie ametoa kiasi gani cha pesa kwa dada yako, zaidi ya kutuchanganya kifamilia?”
“Lakini mama tuachane na hayo, kaburi la babu na bibi nalifahamu, kaburi la kaka mkubwa nalifahamu. Makaburi yote yanayotuhusu nayafahamu na kila mwisho wa mwaka huenda kuyazuru familia yote na pia huenda kila mwezi kusafisha na kuyaweka katika hali ya usafi. Lakini kaburi la dada Monika lipo wapi, japo sikuhudhuria mazishi yake?”
“Masalu, wee mtoto mdogo hujui lolote, elewa kuwa dada yako Monika amefariki.”
“Mama, bado hayajaniingia akilini.”
“Masalu hebu niondokee, nilifikiri jambo la maana kumbe ni upumbavu,” mama alisema huku akijiandaa kurudi shambani.
“Mama unaniona mtoto lakini mambo yetu yote yapo hadharani.”
“Mambo gani?” Mama alishtuka na kunigeukia ili kutaka kujua.
“Dada Monika alinieleza mengi kuhusiana kifo chake alichotishiwa na baba kwa ajili ya kukikataa kidonda na kunitisha kidonda kile kitahamia kwangu.”
“Masalu nikueleze mara ngapi kuwa dada yako Monika alikuwa muongo aliyetaka aonekane alichokifanya ni sahihi cha ukosefu wa adabu?”
“Lakini mama mbona mengi aliyonieleza yanatokea? Uongo wake ni nini?”
“Kama nini?”
“Kuhusu wewe kuteseka na kilimo wakati familia ina uwezo mkubwa?”
”Kulima si kujitesa bali kujipa mazoezi.
“Mama, juzi uligombana na baba akikulazimisha uje shamba wakati ulikuwa hujisikii vizuri hata juzi uliniambia hukulala kutokana na maumivu ya mgongo. Mama naona umejisahau pale uliponiambia kuwa baba atakuua kwa vitu vya kulazimishana, bado tu unasema mazoezi. Mama unaweza kuona mnafanya siri lakini kila kitu kipo wazi.
“Unaweza kuona watu wapo kimya, lakini kuna maneno mengi sana juu ya kifo cha dada Monika, hakina tofauti na kifo cha mtoto wa dada Mihayo.”
“Masalu! Hakina tofauti ya nini?”
“Wanasema hata mtoto wa dada Mihayo alipokufa hakuzikwa.”
“Hakuzikwa alifanywa nini?” Maskini mama aliniuliza huku macho yakimtoka pima na kijasho chembamba kilimvuja.
“Eti wanasema kile chumba ambacho hakifunguliwi ndani kuna maiti ya mtoto ambayo huwa mnaipaka mafuta kila siku ndicho chanzo cha dada Mihayo kuwa na utajiri mkubwa kuliko wenzake.”
“Wee mtoto, haya yote umeyasikia wapi?” Mama alishtuka.
“Shemeji aliniambia kuwa kabla dada hajakata roho alimueleza mambo mengi juu ya ushirikina wa familia yetu kutumia kidonda chake kujipatia utajiri na hata alipotoka nyumbani kukataa kuendelea na kidonda ilisababisha kifo chake.”
“Masalu! Alimueleza kuwa kwenye chumba hicho kuna maiti ya mtoto?”
“Ndiyo, tena alimueleza kuwa watu waliokuwa wakiipaka maiti ile mafuta ni wewe baba na yeye dada Monika.”
“Mungu wangu, kayasema hayo Monika?”
“Na wasiwasi mwingine wanasema maiti ya dada Monika huenda nayo haikuzikwa imefichwa kwenye chumba kile cha siri.”
“Ooh... Mungu wangu ...Ooh moyo wangu,” mama alisema huku akishikilia kifua na kuanguka chini. Nilipojaribu kumuamsha hakuamka, nilipiga kelele kwa majirani wa shamba la pili. Sauti yangu iliwakusanya watu ambao walifika na kumpa huduma ya kwanza mama aliyekuwa amepoteza fahamu.
Alipopata fahamu aliwaomba wampe msaada wa kumrudisha nyumbani, jirani yetu mama Kusekwa alimsindikiza mama hadi nyumbani. Tulipofika alituacha na yeye kurudi shambani. Nilijawa na wasiwasi huku nikijilaumu kwa kumueleza mama mambo ambayo niliyaona mazito.
Nikiwa pembeni ya mama aliyekuwa bado amejilaza kwenye zulia huku akipuliziwa na upepo wa feni aliniita:
“Masalu.”
“Naam mama.”
“Kuna mtu aliuliza sababu ya kuanguka kwangu?”
“Ndiyo mama.”
“Uliwajibu nini?”
“Niliwaeleza kuwa ulianguka ghafla.”
“Hawakukuhoji zaidi?”
“Hawakunihoji zaidi ya kukupa huduma ya haraka.”
“Ooh, afadhali.”
“Unajisikiaje kwa sasa?” Nilimuuliza mama kwa huruma.
“Mmh, sijambo kidogo ila nakuomba tuliyozungumza yote usimwambie mtu.”
“Sawa mama.”
Nilimkubalia ili tu kuiacha siku ile ipite pia kutokana na hali yake, lakini bado sikupata jibu la dada Monika amekufa kweli, japo shemeji alinihakikishia amekufa. Na kama amekufa amezikwa wapi au ndiyo yaleyale niliyoelezwa kuwa mwili wake umefichwa ndani.
Moyoni nilibakia njia panda kutaka kujua ukweli kuhusu dada Monika, nilipanga kama mama atashindwa kunieleza basi nitamvaa baba na ukali wake ili nijue amekufa au mzima na kama amekufa amezikwa wapi.
Sikutaka kuliulizia jambo lile haraka kutokana na hali ya mama, niliamua kukaa kimya, lakini moyoni sikuwa na raha kutaka kujua ukweli wa kifo cha dada Monika. Siku moja asubuhi kabla ya kwenda shule mama alinifuata chumbani kwangu na kunieleza nisiende shule kuna sehemu anataka kunituma.
Nilibadilisha nguo zangu za shule na kuvaa za nyumbani, wakati huo alikuwa akijiandaa kwenda shambani. Lakini siku ile hakuwahi kama ilivyo kawaida yake. Tuliondoka nyumbani pamoja kuelekea shambani, baada ya muda wa chai, kutoka  nyumbani mpaka shambani ni mwendo wa dakika 45. Tulikwenda huku tukizungumza, mama aliniulizia habari za shule, nilimuelezea maendeleo yangu japo hakuwahi hata siku moja kushika madaftari yangu kuyaangalia.
Katika kumbukumbu zangu nilielezwa kuwa mama aliishia darasa la sita baada ya kupewa ujauzito na baba kisha kumtorosha. Taarifa hizo alinipa marehemu ambaye sina uhakika kama kweli amekufa au maiti yake imefungiwa katika chumba kisichofunguliwa.
Dada Monika alinieleza kuwa mama yetu alitengwa na familia yake baada ya kubebeshwa ujauzito na baba na kutoroshwa. Kitendo kile ndicho kilichofanya mama aishi maisha ya peke yake bila ndugu, ndugu yake mkubwa alikuwa baba kitu kilichofanya amnyanyase kwa kujua hana pa kwenda.
Sababu ile ndiyo iliyomfanya mama aishi kama mtumwa kwa vile kila alipofanya kosa baba alimtishia kumfukuza. Kwa kweli kitendo cha baba nilikiona cha kikatili sana, kila dakika nilijikuta nikimchukia baba kwa roho mbaya ya kuitesa familia yake kwa ajili ya mali.
Niliamini  mateso ya muda mrefu na shuluba zote, baada ya kupata utajiri wa kushirikina, basi alitakiwa mama atulie na kufaidi matunda ya uchawi wao. Lakini imekuwa tofauti mama kila kukicha amekuwa mtu wa kusurubika. Kilichonishangaza ni ndugu zangu kushindwa kumsimamia mama na kumpunguzia mateso ya kulima na kupasua kuni. Kila nilipomtazama mama yangu roho iliniuma na kujiapiza kama Mungu atanisaidia kupata kazi na kuwa na maisha mazuri basi nitamuondoa kwa baba.
Moyoni nilijiapiza kutokubali kuishi maisha machafu ya ndugu zangu ya kutoa familia zao kwa ajili ya kafara ya hatari na kujiona kama wataishi milele. Nilijiuliza dada Mihayo atamwambia nini mwanaye mbele ya Mungu, aliyemtoa kafara kwa ajili ya utajiri na baadaye kuendelea kumtesa kwa kumlaza kwenye chumba?
                                                             ****
Kuna kitu alinieleza dada Monika juu ya mama na kuniomba nimchunguze, nakumbuka siku hiyo alinieleza:
“Masalu, mama yetu anaishi maisha ya mateso makubwa sana, baba ni shetani asiyefaa mbele ya jamii. Nataka nikueleze kitu kimoja ambacho mimi wananikataza. Kwa taarifa yako nilikatazwa kulala na mwanaume lakini baba ana mwanamke kamjengea nyumba ya gharofa moja.”
Dada Monika aliendelea kunieleza jinsi watu wanavyotumia pesa huku mama akiteseka, alinieleza:
“Mdogo wangu familia yetu yote tutateketea kwa moto wa kiama, hebu ona maisha ya mama yanalingana na utajiri tulionao? Hata kama kuyumba hatuwezi kuishiwa kiasi cha kutisha, sawa na tembo kuugua maralia hawezi kukonda kama mbwa.
“Masalu, sema tu mama mbishi, nilimueleza mapema tuondoke pamoja ili aepukane na maisha ya mateso, lakini mama kama amerogwa na baba haelewi hasikii. Hivi kweli mama yetu ni wakuvaa kandambili za kufunga na kamba?” Nakumbuka siku hiyo dada Monika alizungumza huku akibubujikwa machozi.
Mama anateseka dada Mihayo anamhonga bwana wa pembeni gari, Masalu inauma lakini sina uwezo. Kama kidonda hiki angekuwa nacho mtu mwingine na mimi kuwa na uwezo wa dada Mihayo hata kwa kutoa kafara ya mtoto mama yangu angeishi kama malaika.
Lakini sina uwezo, hata hiki kidogo ninachokipata nikimpelekea mama hatakitumia zaidi ya kugeuzwa ndondocha na baba.”                                                            
Kila nilipoyakumbuka maneno ya dada nilijikuta nikitokwa na machozi. Nilikumbuka neno moja ambalo dada Monika alinieleza nilifanyie kazi, aliniambia:
“Masalu, mchunguze mama muda mwingi akiwa peke yake mkono huwa shavuni, na kama utamfuatilia kwa muda baada ya kutoa mkono shavuni hutikisa kichwa na kufuta machozi. Katika maisha yetu toka tupate utajiri wa kishirikina furaha ya mama imetoweka, kutabasamu kumekuwa kama ajali lakini kulia kumekuwa kitu cha kawaida.
Mara nyingi mama amekuwa kila akiwa peke yake kanga huwa mkononi ili kufuta machozi. Vitu vile nilivifanyia kazi na kumueleza dada Monika yote aliyonieleza ni kweli. Aliniuliza swali lingine:
“Masalu umeshawahi kumuona mama akivaa nguo mpya?”
“Hapana,” nilimjibu.
“Hebu jifikirie mama yetu ni wa kuvaa nguo zilizoachwa na wanaye?”
“Nilikuwa sijui.”
“Kama hujui, hata macho yako hayaoni? Masalu sasa hivi wewe si mtoto unaona vitu ambavyo baadaye vinataka majibu kwa kile ulichokiona.”
“Huwezi kuamini dada nilikuwa kama nimefungwa akili, unachonieleza sasa hivi ndiyo kama kwangu kunapambazuka baada ya kukaa gizani kwa muda mrefu. Kama usingenieleza haya ningekufa kibudu.”
Niliamini kabisa kama dada Monika kweli amekufa, basi alikuwa amekufa na mengi moyoni sawa na samaki mwenye mengi ya kuzungumza lakini kila alipofumbua mdomo maji yalimjaa mdomoni. Kama alivyonieleza shemeji kabla ya kufa kutokana na maelezo yake mengi angenieleza mengi mazito.
                                                        ****
Tulipofika shambani mama hakuonesha kama anataka kulima, aliniweka chini ya mti huku akionekana mwingi wa mawazo. Baada ya ukimya mfupi mama aliniita jina langu.
“Masalu.”
“Naam mama.”
“Najua umesikia mengi juu ya maisha yetu, lakini hakuna ukweli kwa yote uliyosikia nakuomba uwapuuze, sawa baba.”
“Lakini mama mbona yote niliyoelezwa yana ukweli.”
“Ukweli upi?
”Mama kwanza naanza na wewe, toka nipate akili sijawahi kukuona ukifurahi, kila siku mtu wa masikitiko na kutokwa na machozi.”
“Ha! Masalu umejuaje?”
“Mama dada Monika kanieleza mambo mengi sana ambayo niliyafanyia kazi na kuupata ukweli juu yako.”
“Ukweli gani?”
“Kuhusu muda mwingi kuweka mkono shavuni na kutokwa na machozi, nilikufuatilia bila wewe kujijua na kuupata ukweli, pia uvaaji wako wa nguo mama toka nipate akili sijakuona ukivaa nguo mpya au nzuri, pia mama hebu angalia ndala zako. Kwa maisha tunayoishi wewe si wa kuvaa ndala za kufunga na waya.”
Niliposema vile mama alijiangalia kama hakujua alichokivaa wakati wa kutoka nyumbani.
“Mama najua yote haya yanatokea kwa ajili ya nini.”
“Kwa ajili gani?”
“Haya ni mateso anayokupa baba, baada ya kutengwa na ndugu zako, na chanzo cha yote ni yeye. Kutokuwa na ukaribu na familia yako, katumia ni fimbo ya kukuadhibia. Hivi mama hata wanao wengine wanajijali wao na kukusahau , bila wewe wangeijuaje dunia?
“Mama maisha haya unayoishi siyo mazuri, nilisikia eti baba alikutishia maisha kama utataka mambo makubwa. Haya ndiyo aliyoyakataa dada Monika kidonda akitunze yeye wengine wale maisha mazuri. Matokeo yake mnaamua kumuua na kuificha maiti yake.”
“Masalu nani kaificha maiti ya Monika?”
“Ipo wapi?”
“Masalu swali gani hilo, kila anayekufa si huzikwa?”
“Mbona mtoto wa dada Mihayo hakuzikwa?”
“Masalu una uhakika gani?”
“Dada Monika hakunificha yote nisemayo ni yeye aliyeniambia ni mengi sana nayajua kuliko mtu mwingine.”
“Masalu yote usemayo ni kweli, nakuomba usimwambie mtu yoyote habari hizi.”
“Kama ni kweli naomba kuanzia leo kazi ya kulima aachiwe mtu mwingine, uvae nguo nzuri ili ulingane na utajiri wa familia yetu.”
“Masalu hilo haliwezekani.”
“Kwa nini?”
“Baba  yako ataniua, naomba mwanangu yote unayoyaona yaache kama yalivyo, na ukizidi kumchokonoa anaweza kukuua.”
“Kama alivyomuua dada Monika?”
“Usiseme hivyo Masalu.”
“Mama tunafichana nini? Hivi utajiri ndiyo unaotufanya tukose huruma kwa wenzetu?”
“Masalu nakuomba usichimbe sana.”
“Hapana mama, huwezi kujua sasa hivi tunaonekana vipi mbele ya macho ya watu, kwa taarifa yako inasemekana Monika hajazikwa amewekwa ndani kwa imani za kishirikina.”
“Nani kasema?”
“Aliyekuwa akikaa na dada Monika ndiye anayeeneza habari hizi.”
“Yeye kajuaje?”
“Mama ina maana ninapozungumza na wewe unakuwa wapi? Nilikueleza kuwa kabla ya kufa dada Monika alimpa siri kubwa ya maisha yetu na sababu ya kifo chake. Pia alimueleza kuwa alikuwa na siri nzito ambayo asingemwambia mtu zaidi yangu mimi.”
 “Mmh, sasa huyo kijana kinamhusu nini kututangaza vibaya?”
“Kinachomuuma ni kumuulia mtoto wake asiye na hatia.”
“Hivi baba yako akijua kuwa ndiye anayetutangaza vibaya kwa watu kutakuwa na usalama kweli?”
“Atamfanya nini?”
“Masalu wee acha baba yako hana dogo, anaweza hata kumkata kichwa.”
“Akimuua atapata faida gani? Si ndiyo atakuwa anaongeza chuki kwa watu?”
“Masalu mwanangu, kwa umri wako hata nikueleza kitu hutanielewa, nakuomba kila ulilosikia liache lilivyo, wewe bado mtoto mdogo litakuchanganya.”
“Sawa nimekuelewa, ila naomba ukweli wa jambo moja.”
“Jambo gani?”
”Kuhusu ukweli wa dada Monika.”
“Ukweli upi?”
”Ni kweli amekufa?”
“Ndiyo.”
“Amezikwa wapi?”
“Mmh! Si makaburini.”
“Makaburini gani?”
“Kwa kweli siwezi kujua makaburi gani sikwenda kuzika.”
“Mama kuna makaburi tofauti na tuliyoyazoea?”
“Hakuna.”
“Na misiba yote huanzia kanisani kisha kupelekwa kuzikwa?”
“Ndiyo.”
“Sasa msiba wa dada Monika mliupeleka kanisa gani?”
“Masalu hata ukijua itakusaidia nini?  Aliyekufa amekufa huwezi kumfufua.”
“Hata kama siwezi kumfufua, dada Monika ndiye kipenzi changu, kaburi lake kwangu ni kielelezo cha kumuona kipenzi changu.”
“Masalu nakuomba suala hilo uachane nalo.”
“Yote nitaachana nayo si la dada Monika.”
“Masalu ukitaka kujua mengi utakosana na baba yako.”
“Kwa hiyo ukweli dada Monika maiti yake haikuzikwa?”
“Masalu nakuomba mwanangu chondechonde achana na hayo ili maisha yako yawe salama.”
“Kwa hiyo nikitaka kujua baba ataniua?”
“Hawezi kukuua ila utakuwa matatizoni.”
“Mmh! Sawa mama,” nilikubali kwa shingo upande kutokana na kuonekana kumuweka mama katika wakati mgumu.
Sikutaka kumsumbua sana mama yangu kutokana na maelezo ya dada Monika, kila nilipomtazama nilimuonea huruma. Nilimuahidi mama toka moyoni mwangu sitaulizia lolote kuhusiana na dada Monika wala kitu chochote kuhusiana na familia yetu.
Kauli yangu ilimfurahisha mama na kuonekana hawezi kuamini nilichokisema.
“Kweli Masalu.”
“Kweli mama, nakupenda sana mama yangu.”
“Asante Masalu, nakuomba kila unachokijua huenda hata mimi mama yako sivijui kwa vile baba yako alimpenda sana Monika hata siri zingine sizijui ambazo alikueleza wewe na pengine kabla ya kufa angekueleza,” maskini mama yangu alisema huku akitokwa na machozi, kitu kilichozidi kuniumiza nami machozi yalianza kunitoka kwa mbali.
“Nimekuelewa mama yangu, nimekuelewa sina budi kukusikiliza.”
“Asante Masalu, siku zote niliamini wewe na Monika ndiyo watoto wangu wanaonijali, endelea kunijali mwanangu wewe ndiye tegemeo langu, soma unikomboe.”
“Nitafanya hivyo mama yangu, nakuahidi kuwa kimbilio lako.”
“Asante mwanangu.”
Baada ya mazungumzo marefu tulirudi nyumbani, lakini  bado aliniacha na maswali lukuki moyoni mwangu, nilijikuta nakubaliana na shemeji, bwana wa Monika kuwa mwili wa dada umefichwa ndani pamoja na mtoto wa dada Mihayo.
                                                SIKU TATU BAADAYE
Siku tatu baadaye nilipata taarifa za kusikitisha za kifo cha utata cha shemeji aliyekuwa bwana wa Monika. Taarifa zilizonitisha na kuamini mazungumzo yangu na mama juu ya taarifa zinazosambazwa na shemeji zilimfikia baba na kuamua kufanya umaruhuni wake.
Ndugu walisema aliporudi nyumbani alianza kusema anasumbuliwa na kichwa huku akisema kama akifa atakuwa ni baba. Na usiku alipiga kelele akilitaja jina la baba, kitu kilichozidi kuaminisha kwamba anahusika moja kwa moja ili kumkomoa baada ya kusikia akitutangazia sifa mbaya familia yetu.
Kifo kile kiliongeza sifa mbaya kufikia hatua familia ya aliyekuwa mpenzi wa marehemu dada Monika kuja kutushambulia kwa maneno ya kutuita wachawi. Siku hiyo nilikuwepo, mama wa marehemu alikuja nyumbani na kuanza kutoa shutuma nzito kwa sauti ya juu huku watu wakisikiliza.”
“Mmeniulia mwanangu kwa imani zenu za kichawi ili muwe matajiri, kumuua mtoto wa Mihayo hamkuridhika mmemuua Monika na kumficha ndani bado tu mmeona haitoshi mmemuua mwanangu. Nawaambia damu ya mwanangu haiendi bure.”
Taarifa zile zilipelekwa kwa baba ambaye aliita polisi na kumchukua yule mama na kumpeleka kituoni. Kwa kweli kilichoendelea sikujua zaidi ya kumsikia baba akitamba atamuonesha. Pamoja na yule mama kupelekwa polisi familia yetu ilitawaliwa na sifa mbaya ambazo wengi walizisikia na kuzisambaza kwa watu kuwa maisha yetu yametawaliwa na utajiri wa kishirikina ambao ulikuwa ukipitia kwenye kidonda cha marehemu dada.
Nilijikuta nikiishi maisha ya kukosa amani, hata tembea yangu ilikuwa ya mashaka kwa kuhofia maneno ya watu. Siku zilikatika walisema mchana, usiku wakalala. Walizungumza sana mwisho wakanyamaza na kusahaulika na maisha yakaendelea.
Katika maisha yetu hakuna kilichobadilika, nilimaliza kidato cha nne kwa kupata matokeo mabaya. Niliamini kufanya vibaya kulitokana na migongano ya mawazo iliyotokana na kuchanganywa na mambo yote yaliyotokea yakihusu familia yetu, na taarifa nilizopewa na dada Monika juu ya kifo chake na matukio mengi ya kishirikina yaliyoilenga familia yetu.
Wazo la kurudia mtihani wa kidato cha nne, lilipingwa na baba na kusema atanipatia shughuli nyingine. Roho iliniuma kwani ndoto zangu zilikuwa kusoma kwa bidii ili siku moja nimkomboe mama kwenye mateso ya kuwekwa kifungoni na baba.
Miezi sita baada ya matokeo mabaya ya kidato cha nne, baba alionesha mapenzi makubwa kwangu tofauti na zamani. Alifikia hatua ya kuzunguka nami kila kona kwenye shughuli zake. Siku nyingine alinipa pesa za matumizi ambazo alinieleza ninunue kitu chochote nikitakacho.
Kwa akili za kitoto nilianza kubadilika na kuyaona yote niliyoelezwa juu ya ukatili wa baba ni uongo. Baba alikuwa mtu mzuri kwa kuninunulia nguo za thamani, nilionekana kweli mtoto wa mtu mwenye pesa tofauti na mwanzo nilivyokuwa nasoma shule.
Baba siku zote alinisifia kuwa mimi ndiye mtoto anipendaye kuliko wote, kauli zile za baba zilinifanya nisahau hata wazo la kumuuliza juu ya dada Monika. Siku moja tulikuwa tumekaa kwenye moja ya hoteli ya baba huku akiniruhusu kula nikitakacho, baada ya chakula baba alinichukua na kuingia naye kwenye ofisi yake iliyokuwa ndani ya hoteli ile ambayo sikuwahi kuingia siku za nyuma.
Baada ya kuingia ofisini baba aliendelea kunimwagia sifa.
“Masalu unajua nakupenda sana kuliko watoto wangu wote.”
“Najua baba.”
“Hebu niambie unataka nini nikufanyie ili ujue napenda sana.”
“Cha kwanza kunipa nafasi ya kurudia masomo niliyoanguka katika mtihani wangu ili nifanye vizuri, bado nina hamu ya kuendelea kusoma.”
“Tofauti na hilo?”
“Siwezi kusema kwa sasa mpaka nitakapofanya mtihani wangu wa marudio.”
“Masalu, kusoma si muhimu sana kwako, kama pesa zipo nitakufungulia mradi wako ili uendeleze maisha yako.”
“Lakini...”
“Masalu hakuna haja ya kubishana, naomba ujiandae kuna duka moja nimelifungua na kuanza kazi wewe ndiye msimamizi mkubwa.“
Nilijikuta nakosa cha kuzungumza na kukubaliana na baba japo nafsi yangu ilitaka kusoma ili nimkomboe mama yangu. Nilijua kukubali mradi ule japo utakuwa chini yangu bado utakuwa wa nguvu za kishirikina kwa kuhofia huenda siku za mbele baada ya kuoa na kupata mtoto akatolewa kafara.
Baba alinitolea hati za kumiliki duka lile lenye jina langu na kunionesha sehemu ya kusaini. Nilisaini na kuniahidi kunifanyia mambo makubwa kuliko ndugu zangu wote. Baada ya kutoka pale aliniingiza kwenye gari lake na kunipeleka mjini Barabara ya Pamba kwenye duka langu.
Nililikuta duka lipo wazi na watu wakiendelea na mauzo ya vitu, lilikuwa duka kubwa la kuuza vitu vya jumla na rejareja. Tulipofika dada mmoja ambaye alikuwa akinifahamu aliniuliza:
“Leo Masalu ndiyo umeamua kuja?”
“Alikuwa anamalizia masomo,” baba alijibu.
“Karibu bosi.”
“Asante.”
Nilijibu huku nikiingia dukani na kwenda kukaa kwenye kiti changu kilichoandaliwa kwa ajili ya kukalia niwapo kazini. Baada ya kukagua duka lililokuwa likilingana na maduka ya  ndugu zangu, baba aliondoka na kuniacha nisimamie duka langu.
Alinipitia jioni na kunirudisha nyumbani, nilipofika nyumbani nilimueleza mama kuwa nimepewa duka na baba. Ajabu mama badala ya kufurahi alitokwa na machozi, kwa vile tulikuwa peke yetu nilimuuliza:
“Mama unalilia nini?”
“Mmh, najua hukufurahi na unaweza usifurahi.”
“Kwa nini mama?”
“Ni vigumu kunielewa kwa sasa lakini tumuombe Mungu aepushe mbali.”
“Mama mbona sikuelewi?”
“Suala la shule limeishia wapi?”
“Baba amekataa na kusema tayari ameishanifungulia duka, na leo ndiyo nimekabidhiwa rasmi.”
“Mmh! Haya”
“Kwani  kuna nini?”
“Hakuna ubaya.”
“Mama kuna kitu hutaki kuniambia.”
“Hakuna kitu kikubwa zaidi ya kukatika kwa ndoto yako ya kusoma.”
“Mama nitasoma tu.”
“Kwa duka lako, si unawaona ndugu zako walivyo bize na maduka yao hata muda wa kunikumbuka hawana.”
“Mama nitajipanga, siku hizi kuna masomo ya jioni.”
Siku zilikatika, biashara nayo ilizidi kushika kasi, hata mwili wangu ulibadilika na kuonekana mtu mzima kutokana na kunenepa, hata sauti yangu ilibadilika. Lakini ilikuwa tofauti na wenzangu, mimi nilibakia nyumbani na mama pamoja na mfanyakazi mmoja, niliamua kumpumzisha mama kazi za shamba, lakini mama aling’ang’ania kwa kusema kama akiacha kwenda shamba atafukuzwa na baba.
Nilipomuuliza baba naye alinijia juu na kunionya nisiingilie mambo yake, sikuwa na jinsi, nilimuacha mama aendelee kulima huku nikitumia vijana kumsaidia mama, ambaye alifanya kazi ndogondogo. Kingine ambacho sikukubaliana na baba ni kuhusu mavazi ya mama yaliyokuwa yamechoka.
Hapo sikukubali hata kidogo na nilikuwa tayari kwa lolote.
“Masalu unataka tubishane?” baba alinikaripia.
“Kwa hili baba sikubaliani nawe hata kidogo.”
“Umeanza kuvimba kichwa kwa vipesa unavyopata?”
“Si kuvimba kichwa, nipo sahihi, kama mali zako chukua lakini nimechoka kuiona hali hii mpaka lini?”
Sikuogopa chochote cha baba mpaka tulipokubaliana kumnunulia mama nguo mpya, pamoja na mzozano huo bado baba hakuonekana kukasirika sana. Mama alibadilika  na  kuanza kuvaa vitenge vya gharama, hata kandambili alivaa mpya.
Ndugu zangu walipokuja nyumbani hawakuamini kumkuta mama yetu kapendeza. Walipomuuliza aliwaeleza ni kwa ajili yangu, walinifuata kutaka kujua nimewezaje kumbadili baba kukubali mama kuvaa nguo mpya. Niliwaeleza ni msimamo hakuna kitu kingine, maisha yaliendelea.
Katika vitu ambavyo baba alinionya ni kutembea na wanawake, nilikumbuka kauli za dada Monika kuwa alianza kuelezwa asijihusishe na wanaume na mwisho alipata kidonda cha kichawi.
Nilimkubalia kumridhisha tu, lakini niliendelea kuwa na uhusiano na binti mmoja ambaye ndiye tuliyepanga kuoana siku za mbeleni. Siku zote mambo yangu nilikuwa nayafanya kwa siri kubwa bila baba kujua kwa kuamini sina uhusiano wa kimapenzi na mwanamke.                                                      
                                                                           ****
Siku moja nikiwa nimelala niliota kitu kama nyoka, lakini sikukielewa vizuri kikiniuma kwenye mguu wa kulia kwa ndani. Nilishtuka lakini hakukuwa na kitu chochote, niliendelea kulala. Kesho yake nilikwenda dukani kama kawaida na kuendelea na shughuli zangu.
Wiki moja baadaye nilianza kusikia muwasho sehemu niliyoota nimeumwa na kitu kama nyoka. Nilimueleza mama asubuhi baada ya kujikuna mpaka kukaleta weusi sehemu iliyokuwa ikiniwasha. Mama alishtuka, jambo lililonitisha.
”Mama mbona umeshtuka?”
“Baba yako alikueleza nini?”
“Kuhusu nini?”
“Huo muwasho wako?”
“Hata, sijazungumza lolote.”
“ Mmh!” Mama aliguna.
“Unaguna nini?” nilimuuliza.
“Hapana.”
“Mbona kama unanitisha, unakuwa hauna tofauti na wa dada Monika?”
“Ni kweli.”
“Unataka kuniambia ndiyo huu?”
“Ndiyo.”
“Mungu wangu nimekwisha.”
“Wala hujaisha, ukifuata masharti yake hauna tatizo.”
“Kwa hiyo na mimi nitakuwa na kidonda kama dada Monika?”
“Ndiyo lakini hakiumi.”
“Na nikikosea nitakufa kama dada Monika?”
“Monika kafa na yake.”
“Mamaa, juzi tulizungumza nini, leo unanibadilikia?” Nilimuona mama akitaka kuficha mambo.
“Masalu nakuomba suala hili muulize baba yako na usimueleze kuwa tumezungumza.”
“Sawa mama.”
Niliachana na mama huku mwili wote ukininyong’ea kwa kujua niliyoelezwa na dada Monika yametimia.
Siku ile hata hamu ya kwenda kwenye duka langu sikuwa nayo, kwa kuamini nilikuwa nimeishaharibika. Nilishinda ndani huku nikilia lakini mama alitumia muda wake kunibembeleza kuwa sijaharibika kama ninavyo fikiria.
“Masalu usilie mwanangu.”
“Mama kwa nini mnanitendea unyama kama huu kosa langu nini?”
“Huna kosa mwanangu, kidonda hiki humfuata yule aliyeteuliwa na mizimu.”
“Wataniteua vipi wakati mimi sitaki?”
“Huwezi kukataa.”
“Mama nina malengo yangu wewe unajua.”
“Ni kweli, lakini hakuna wa kumzuia baba yako uamuzi wake.”
“Mama na mimi nitakufa kama dada Monika?”
“Kwa nini?”
”Siwezi kufuata masharti ni magumu.”
“Si magumu ukizingatia.”
“Siwezi mama siwezi...,” nilikatwa kauli na sauti ya baba aliyekuwa akimwita mama. Nilimuona mama akishtuka na kuanza kutetemeka na kijasho chembamba kilimvuja.
“Mama vipi?”
“Naomba usimwambie baba yako niliyokueleza, ataniua.”
“Siwezi kumwambia.”
“Ng’wana Manoni.”
“Lama,” mama aliitikia huku akitoka chumbani kwangu.
“Vipi mbona unatoka chumbani kwa mtoto?”
“Hajisikii vizuri.”
“Na shamba hujaenda?”
“Baba Mihayo nimwache Masalu anaumwa niende shamba?”
“Kwani anaumwa sana?”
“Toka asubuhi analia tu.”
“Kafanya nini?”
“Mmh, nenda ndani ukamuone.”
“Masalu,” baba aliniita.
“Naam baba.”
“Eti kuna nini?”
“Kuna vitu ambavyo sielewi.”
“Vitu gani?” Baba alisema huku akiingia ndani.
Alipoingia ndani alinikuta nimeshikilia mguu.
“Kuna nini?”
“Baba sehemu hii inaniwasha sana kufikia hatua ya kunikosesha raha.”
“Hebu nione,” nilimuonesha baba, baada ya kuona alisema:
“Kumbe hiki?”
“Ndiyo baba.”
“Sasa tatizo nini?”
“Kinaniwasha.”
“Usikikune kitapoa chenyewe.”
“Hapana baba bora niende hospitali.”
“Masalu usiende hospitali, ugonjwa juu si wa kawaida.”
“Wa nini?”
“Utajua tu baadaye, lakini chonde usiende hospitali.”
“Au ndiyo kama wa dada Monika?”
“Eti?” Kauli yangu ilimshtua baba na kunitazama mara mbili kama ndiyo siku yangu ya kwanza kuniona.
“Eti umesemaje?”
“Baba mbona umeshtuka hivyo?”
“Sijakuelewa, hebu rudia swali lako.”
“Nauliza, kisiwe kidonda kama cha dada Monika.”
“Mama yako ndiyo kwakwambia? Leo atanitambua,” baba alikuja juu.
“Baba badala ya kunijibu swali langu unakimbilia kutaka kumpiga mama au ndiyo umemuona gunia lako la mazoezi,” nilizidi kumchanganya baba na maneno yangu ambayo hakufikiria hata siku moja nitayatamka.
“Masalu mbona unanikosea heshima?”
“Sijakukosea heshima ila nataka kujua ukweli wa muwasho huu kwa vile nilibashiliwa kipindi kirefu.”
“Na nani?”
“Na dada Monika”
“Alikubashiria nini?”
“Alinieleza kuwa kifo chake kimetokana na kukikataa kidonda hiki, na ulichomuahidi ndicho kilichotokea.”
“Muongo, unamsingizia Monika wakati uongo wote kakupa mama yako.”
“Baba utamuonea mama bure, mama hajanieleza chochote zaidi ya kunifanya mtoto mdogo mambo ninayoyajua.”
“Mambo gani?”
“Kuhusu chanzo cha utajiri kidonda cha dada Monika mpaka kifo chake kilisababishwa nini na utabiri wake kidonda kikitoka kwake kinakuja kwangu.”
“Mmh,” baba aliguna, kisha alinitazama kwa muda na kuangalia juu kabla ya kushusha tena pumzi.
“Masalu.”
“Naam.”
“Niambie ukweli mama yako kakuambia nini juu ya huu muwasho?”
“Kaniambia ni muwasho wa kawaida, utapoa wenyewe.”
“Hakukuambia kitu kingine?”
“Hajaniambia, ndiyo maana nilijua ananidanganya, dada Monika alinipa siri nyingi, zingine hata mama hajui na bahati mbaya wakati anakufa nilikuwa mbali lakini kuna mengi mazito alitaka kunipa juu ya familia yetu.”
“Monika alikuambia nini?”
“Alinieleza jinsi kidonda chake kilivyoanza kama muwasho na mwisho kilikuwa kidonda kisichouma zaidi ya kutoka maji na kukatazwa asiyafute.”
“Mmh, pamoja na uongo wake nakuomba usimuamini ni mfitini yule.”
“Baba unataka kunihakikishia kidonda hiki sio kama cha dada Monika?”
“Nimekueleza usimfuate Monika ni muongo.”
“Kama muongo naomba na mimi uniondolee masharti ya kuwa na mke.”
“Masalu, umri wako bado.”
“Baba mimi si mdogo, ukweli ni kwamba huu muwasho mwisho wake ni kidonda ambacho kitaingiza pesa kwa njia ya kumwagika maji. Baada ya dada Monika kuyashindwa masharti yako uliamua kumuua na mimi nahofia utaniua.”
“Narudia tena kukueleza Monika ni muongo.”
“Baba nasema kama ndicho kidonda hiki basi nami nitakufa kama dada Monika.”
“Masalu kuna sababu ya kuzungumza kwa kituo.”
“Sawa baba lakini kaa ukijua kama muwasho huu mwisho wake ni kidonda cha utajiri sikitaki nakuomba unirudishe shuleni.”
“Nikurudishe shuleni fedha za shule utazipata wapi?”
“Kwani lazima nipate kidonda ili nisome?”
“Utasoma, lakini kumbuka fedha zinatafutwa na njia zake pesa zipo nyingi.”
“Moja wapo ni kidonda changu?”
“Masalu tutazungumza, hebu vaa kuna mali mpya nimeituma dukani mwako twende ukaiangalie.”
 “Sawa baba,” nilikubali shingo upande na kukubali kuondoka na baba kwenda dukani kwangu. Nilipanga kutokwenda dukani baada ya kupata uhakika wa muwasho wangu.
Niliondoka na baba hadi dukani ambako alinionesha baadhi ya bidhaa alizoniagizia toka China, vilikuwa vitu vingi sana ambavyo vilifanya duka langu liongezeke. Kwa muda mfupi hata ndugu zangu walianza kunionea wivu. Wazo la haraka lilikuwa huenda aliyoyafanya dada Monika ya kutaka  naye awe na maisha yake ndiyo yaliyosababisha hali ile.
Hali ya muwasho iliendelea kupungua na kuweka kitu kama gamba kwenye weusi ule. Siku moja asubuhi ilipoamka nilikuta lile gamba limetoka kutokana na kujigeuza na kuweka kidonda. Moyo wangu ulilipuka na kujua kazi imeanza, kutokana na maelezo ya awali kidonda kile hakikutakiwa kutibiwa.
Nilijikuta nikikosa raha pamoja na mali zote alizonipa baba  sikuwa na furaha yoyote moyoni mwangu kuishi na kidonda kisichowekewa dawa mpaka mwisho wa maisha yangu. Nilipoamka na kukuta hali ile nilimweleza mama, naye alinipa jibu jepesi.
“Aliyokueleza dada yako yametimia.”
“Mama nitafanya nini, nitaishi hivi mpaka lini?”
“Masalu, ondoa wasiwasi kama nilivyokueleza toka mwanzo usishtuke sana kwa vile hali hii nilishakueleza mapema uishi vipi baada ya kutokea kwa hali hii.”
“Mama kusema ni rahisi, lakini haivumiliki, nitaishi vipi na watu wakijua nina kidonda kama cha dada Monika nitauweka wapi uso wangu?”
“Nani atajua, labda utawaonesha wewe.”
“Duniani hakuna siri.”
“Ukitaka iwe siri itakuwa siri.”
“Lakini kwa nini umenifanya hivi si mngeniuliza kuliko kunipa kidonda bila idhini yangu?”
“Mimi utanilaumu bure wa kumlalamikia ni baba yako.”
“Mama nami nitakufa kama dada siwezi kuishi maisha ya mipaka.”
Nilimuhakikishia mama sitakubali kuishia maisha yale bali nitakayoamua mwenyewe.
Siku ile mama aliniomba nisivae viatu na soksi bali nivae sandoz ili nisikibughudhi kidonda ambacho kilikuwa kimeanza kutoa maji. Ugumu wa  kuishi maisha ya kidonda nilianza kuuona kwa kuamini mabadiliko yangu ya mavazi lazima watu watataka kujua kumetokea kitu gani kilichosababisha hali ile.
Siku ile nilishinda ndani nikilia japo  mama alijitahidi kunibembeleza, sikuweza kumkubalia niliamini ule ulikuwa uonevu wa kupewa kitu nisichokipenda tena chenye masharti ya kumdhalilisha mtu.
                                                             *****
Taarifa zilimfikia baba aliyekuja kunipoza, alipofika alinikuta nimejifungua ndani kwani sikuwa na hamu ya kuonana na mtu. Alinigongea mlango kwanza nilikaa kimya bila kujibu lolote.
“Masalu hebu fungua tuzungumze.”
Sikumjibu nilikaa kimya, lakini aliendelea kunibembeleza mpaka nilipofungua mlango. Nilipomuona tu niliangua kilio.
“Baba mmenifanya nini?”
“Masalu mwanangu hebu tulia nikueleze jambo.”
“Kitu gani baba utachonieleza nikuelewe?”
“Najua umeshtuka kuona kidonda hicho, nataka kukueleza kila kitu ulichoelezwa na Monika kina ukweli. Lakini nakuomba utusamehe kwa uamuzi wa kidonda hiki kuhamia kwako.”
“Lakini kwa nini hamkunishirikisha mwenyewe?”
“Hatukuwa na jinsi, pia hakuna mtu mwingine katika familia yetu ambaye angeweza kukaa na kidonda hiki baada ya Monika kufa.”
“Baba mimi nitaweza wapi maisha ya mipaka?”
“Unaruhusiwa kufanya lolote kasoro kulala na mwanamke tu.”
“Baba huoni kunikataza kulala na mwanamke ni sawa na kuiondoa furaha yangu moyoni?”
“Kwani usipolala na mwanamke unapungukiwa nini?”
“Vingi baba, vingi sana hakuna raha ya mwanadamu kamili bila kuwa na mwenza.”
“Ni mawazo yako, ukiizoea wala haitakusumbua.”
“Na nikitembea na mwanamke?”
“Utamfuata dada yako Monika.”
“Bora nimfuate,” nilimjibu kwa hasira.
“Hapana usifanye hivyo kuna vitu vingi nilivyopanga kukufanyia kuliko watoto wangu wote, huoni hata sasa hivi wanakuonea wivu? Nakuhakikishia kukufanyia mambo mazuri. Nakuomba usiwe kama dada yako Monika.”
“Sawa baba,” nilikubali kwa shingo upande.
Kukubali kwangu baba alikufurahia sana na kunikumbatia, hakujua jinsi gani mwenzake nilivyoumia. Tuliondoka pamoja kwa maelekezo yaleyale ya mama ya kutovaa viatu na soksi ili kukiacha kidonda kipumue. Nilikubaliana na baba ambaye hakutaka niwe kwenye mawazo sana muda wa siku ile kuwa nami karibu muda wote. 
Nilijilazimisha kuikubali hali ile kwa vile sikuwa na jinsi, hata ningefanya nini isingebadilika. Siku zilikatika huku nikipata maswali mengi kutokana na kubadilika na kuonekana mtu mwenye mawazo mengi. Watu wangu wengi wa karibu walitaka kujua sababu ya mimi kuwa katika hali ile.
Niliwaeleza nipo sawa, lakini hawakukubali na kunikubalia kwa shingo upande,  siku zilikatika huku nikiendelea kuficha siri zangu. Tatizo lililonisumbua lilikuwa kwa mpenzi wangu ambaye siku za nyuma nilikuwa nikifanya naye mapenzi hadi kufikia hatua ya kumuahidi kumuoa.
Mwanzo nilijitahidi kumkwepa ili asijue sababu ya mimi kufanya vile, lakini kila siku nilipozua uongo alinikubali mwisho uongo uliisha.
“Masalu mbona siku hizi sikuelewi?”
“Kivipi?”
“Kila siku umekuwa mtu wa visingizio.”
“Lakini si nimekueleza sababu?”
“Sababu gani hizo?”
“Kwa hiyo unatakaje?”
“Nina hamu na wewe mpenzi wangu.”
“Si nimekueleza subiri mpaka tutakapooana.”
“Masalu usinitanie, si ni wewe uliyenilazimisha tufanye mapenzi kabla ya ndoa?”
“Ni kweli, lakini nimegundua tulifanya kosa.”
“Masalu niambie moja unanipenda hunipendi?”
“Nakupenda.”
“Basi nataka leo tulale pamoja.”
Kwa kweli kwangu ulikuwa mtihani mgumu wa kumkwepa mpenzi wangu nisifanye naye mapenzi. Jioni nilipotoka kazini alinipitia na kwenda La Kailo Hoteli, nilishindwa kumkatalia. Kumbe alikuwa amekwishachukua chumba kabisa, tulipofika tuliingia moja kwa moja ndani.
“Vipi mbona huku?” Nilimuuliza.
“Swali gani hilo Masalu?”
Nilishindwa tena kumueleza kitu chochote, nilibakia kupelekwa kama mkokoteni usio na breki. Tulipoingia ndani mpenzi wangu alionekana na shauku kwa kunivamia kutaka mapenzi. Nilijiuliza nitawezaje kumkatalia tusifanye mapenzi ikiwa tayari ameishalipia chumba?
Nilijiuliza kama nikifanya mapenzi itakuwaje, nilijikuta nikisemea mwenyewe “Liwalo na liwe” niliamua kufanya mapenzi siku ile. Kilichomshtua mpenzi wangu ni kitambaa nilichokuwa nimejifunga mguuni.
“Masalu nini hiki?”
“Niliumia,” nilidanganya.
“Sasa mbona umejifunga kitambaa badala ya dawa?”
“Natumia dawa za asili.”
“Ulifanya nini?”
“Niliumwa na nyoka wa maajabu.”
“Una maana gani?”
“Nilikuwa nimelala ndani nikaota naumwa na nyoka.”
“Enhee.”
“Nilipoamka si ndiyo nikakuta natokwa damu.”
“Mungu wangu, baada ya hapo ikawaje?”
“Nilikimbizwa hospitali, lakini kila dawa niliyowekewa ilizidi kulifanya donda kuzidi kuchimba.”
“Jamani ni nyoka gani huyo akuume kitandani?”
“Hata sijui.”
“Mmekwenda kwa wataalamu wa jadi?”
“Nilikwenda ndiyo natumia tiba yao kidogo sasa sijambo.”
“Walikuambia nini kuhusiana na tatizo lako?”
“Nilielezwa kuwa nitatibiwa hadi nipone.”
“Mmh! Masalu pole sana mpenzi wangu, mbona hukuniambia mapema?”
“Sikupenda kukuumiza moyo mpenzi wangu, nilijua tatizo ni dogo kumbe kubwa.”
“Mmh! Pole sana,” mpenzi wangu aliniambia kwa sauti ya huruma.
“Asante.”
Pamoja na mazungumzo yale, mpenzi wangu alilazimisha tufanye mapenzi kwa vile alikuwa na hamu na mimi sana. Nilijikuta sina jinsi zaidi ya kukubali kufanya naye mapenzi na kukiuka masharti ya baba. Siku hiyo sikurudi nyumbani, nilala hotelini na mpenzi wangu mpaka asubuhi.
Siku ya pili nilirudi nyumbani majira ya saa tatu, mara moja kwenda kubadili nguo kisha niende dukani kwangu. Mama aliponiona alishtuka na kuniuliza:
“Masalu ulikuwa wapi?”
“Nilikwenda kwenye sherehe ya rafiki yangu.”
“Kwa nini hukurudi?”
“Iliisha muda mbaya.”
“Mmh! Sawa baba yako leo hajalala, ninavyozungumza na wewe, ameondoka asubuhi kwenda kukutafuta.”
“Sasa ananitafuta mimi mtoto?”
“Hayo hayajui baba yako, si unajua wewe ndiye mtoto wake wa mwisho.”
“Naelewa, lakini mimi sasa hivi ni mtu mzima.”
“Ina maana jana ulilala na mwanamke?”
“Mama kusema mtu mzima namaanisha kulala na mwanamke?”
“Sina maana hiyo, kulala nje siyo tija, wasiwasi wangu pengine ulimaanisha hivyo.”
“Lakini kumbukeni mnaninyima haki yangu ya msingi.”
“Ni kweli, lakini ndivyo ilivyo, unatakiwa kuvumilia.”
“Hayavumiliki.”
“Tutafanyaje?”
“Ipo siku nami nitapata ufumbuzi wa tatizo langu kama dada Monika.”
“Unataka kufanya kama dada yako? Usifanye hivyo bado tunakuhitaji.”
“Hamna shida na mimi, wenye thamini kwenu ni hao wanaoishi maisha mazuri yasiyo na masharti.”
“Hapana Masalu, utanifanya mama yako nife kwa mawazo. Hujui kiasi gani nilivyokuwa nawapenda wewe na Monika, ndiyo watoto pekee mnaonijali. Baada ya kifo cha Monika umebakia wewe na wewe ukifa nami sitachelewa kufa, sitakuwa na mtetezi wangu wa karibu.”
“Mama nakupenda sana, lakini baba hatutendei haki.”
“Najua tuvumilie, hata wewe si unajua maisha yangu yalivyo?”
”Nayajua mama.”
“Sasa kwa nini unakuwa hivyo, hebu tuvumilie.”
”Sawa mama.”
Nilimkubalia mama lakini moyoni nikiwa na siri nzito ya kitendo nilichokifanya na mpenzi wangu usiku kucha.
Baada ya kujiandaa nilikwenda zangu dukani kwangu, nilipofika nilikuwa tayari wameishafungua. Wahudumu wangu waliponiona walinieleza:
“Bosi mzee alikuja kukutafuta.”
“Amesemaje?”
“Kwa kweli haeleweki, sijui hukulala nyumbani?”
“Kama sikulala nyumbani mimi mtoto?”
“Tutajuaje, tumemkuta kabla ya kufungua duka, alipotuona tu alituuliza upo wapi, sisi tukamjibu tangu jana tulipoachana hatujui upo wapi?”
“Mzee yule anazeeka vibaya, sasa kasemaje?”
7
“Tumemuona akitembea kona moja hadi nyingine kisha alitoweka bila kuaga.”
“Achaneni naye.”
Nilisema huku nikikaa kwenye kiti changu, ajabu wafanyakazi walinishangaa jinsi nilivyoonesha sijali lolote. Haikuchukua muda baba aliingia huku akitweta.
“Masalu.”
“Naam baba, shikamoo.”
“Marahaba, hebu njoo nje mara moja.”
Nilitoka nje kuzungumza na baba, baada ya kusogea pembeni baba aliniuliza.
“Masalu jana ulilala wapi?”
“Kwenye sherehe.”
“Sherehe ya nani?”
“Ya rafiki yangu.”
“Masalu kuna sherehe gani katikati ya wiki?”
“Birthday.”
“Hukulala na mwanamke wewe?”
“Mbona unaniuliza hivyo?”
“Masalu umelala na mwanamke,” baba alinilazimisha.
“Baba nimekueleza nilikuwa kwenye pati unanilazimisha nimelala na mwanamke,” nilijitia kujitetea.
“Masalu tusije kulaumiana, ukirudia tena shauri yako.”
“Hivi baba kwa nini unanilazimisha kitu nisichokifanya, ulinikataza nisitembee na mwanamke si kufanya mambo mengine kama hili la jana, nakushangaa unanitafuta kama mwizi.”
“Mmh sawa.”
“Baba mbona unataka kuninyima uhuru, niliyajua haya toka mwanzo ukabisha, ona sasa unanifuata kila kona,” nilijifanya kulalamika.
“Siyo hivyo, sipendi uingie kwenye matatizo.”
“Baba mi mtu mzima sasa, vilevile najijali.”
“Kama ni hivyo itakuwa vizuri, nisamehe kama nimekukwaza.”
“Nimekusamehe ila naomba uhuru sipendi nifuatwefuatwe.”
Kauli yangu ilimfanya baba azidi kuomba msamaha, tulikubaliana asinifuatilie mambo yangu kwa vile nitajilinda mwenyewe.
                                                              *****
Tangu siku ile hata nilipolala nje baba hakunifuatilia, aliniacha niishi nitakavyo, mpenzi wangu alinishawishi nihame nyumbani ili tuweze kuwa naye siku zote. Nilifikisha wazo kwa baba ambaye mwanzo alipinga lakini  baada ya kumlazimisha alinikubalia kwa shingo upande. Nilipanga chumba maeneo ya Isamilo ambako nilipanga nyumba nzima. Niliendelea na tabia zangu za kufanya mapenzi na mchumba wangu ambaye alihamia kwangu kwa siri.
Siku moja baba alinifuata dukani na kuniita pembeni, baada ya kusogea pembeni aliniuliza:
“Masalu kwa nini hujihurumii?”
“Kivipi?”
“Hebu nione kidonda chako.”
Nilimuonesha, kidonda changu, baada ya kukiangalia alisema:
“Si unaona!”
Nilishangaa, sikujua alisema vile kumaanisha nini? Nilijikuta nikijiuliza kipi kilichomuonesha kitu kilichomshangaza.
“Kuona nini baba?”
“Ina maana huoni kidonda chako kinaonesha hujionei huruma maisha yako.”
“Bado sijakuelewa.”
“Kidonda chako kinatoa maji?”
“Hapana.”
“Unajua kwa nini?”
“Hata sijui.”
“Masalu unatembea na mwanamke wewe.”
“Baba mbona unang’ang’ania neno hilo?”
“Nakuomba uache, shauri zako.”
“Niache vipi wakati sifanyi?”
“Masalu mimi baba yako nimewahi kuona jua kabla yako najua kila kitu, na sababu kubwa ya kuhama nyumbani ni kufanya uchafu wako. Huoni hata biashara sasa hivi zinadoda?”
“Baba tafuteni tatizo lingine siyo mimi.”
“Mmh, haya mama yako asiye kunililia.”
Baba aliondoka akiwa amechanganyikiwa, nami sikuwa tayari kuachana na mpenzi wangu, katika maisha niliamini raha ya mwanaume ni mwanamke na si wingi wa pesa. Siku hiyo hiyo ndugu zangu wote walikuja na kuniweka chini juu ya mimi kuwa na mwanamke.
“Masalu kwa nini hutaki kumsikiliza baba?”
“Nimsikilize kwa lipi?”
“Juu ya wewe kuwa na mwanamke.”
“Mna uhakika gani?”
“Sisi hatuna uhakika ila kasema mwenyewe.”
“Ninyi mna wapenzi?” Niliwauliza.
“Tunao.”
“Sasa mimi nazuiwa na nini?”
“Si unajua hali yako haitaki uwe na mwanamke?”
“Kwa hiyo kidonda niwe nacho mimi maisha mazuri muwe nayo ninyi, sikilizeni kila mtu ataubeba mzigo wake mwenyewe.”
“Masalu utakuja kuijutia kauli yako.”
“Sijutii, mbona dada Monika hakuijutia na mkiniua na ninyi mnafilisika, kazi kwenu.”
Maneno yangu yaliwazima midomo, waliondoka na kuniacha wakiwa hawana hamu na mimi. Tangu siku ile nikawa adui yao mkubwa, niliwashangaa kunikasirikia mimi kuwa na mwanamke wakati wao walikuwa na kila kitu. Kama mateso ya kidonda  nimeyakubali bado hawaridhiki walitaka nikose na raha za dunia.
Ukali wa baba uligonga mwamba, akamtumia mama kunibembeleza, nani msimamo wangu ulikuwa palepale wa kukataa kuwa nalala na mwanamke.
“Masalu jihurumie usije kufa kama dada yako Monika.”
“Mama mkiniua nani atakayebeba kidonda? Dada Monika alinieleza kuwa wote mliotaka kuwapa kidonda mizimu iliwakataa.”
“Ni kweli, lakini unatakiwa uionee huruma familia yako.”
“Mama ninyi hamnionei huruma, mimi nitawaonea vipi?”
“Kumbuka kama utaendelea kufanya kama usipokufa wewe basi utampoteza baba yako.”
“Mama kila mwanadamu hufa kwa ahadi ya Mungu na wala si kwa ajili yangu.”
“Kwa hiyo una mwanamke?”
“Nilikuwa naye lakini sasa hivi kabakia rafiki.”
“Mbona baba yako kaelezwa kuwa unautia mwili wako uchafu ndicho chanzo wa kidonda chako kukauka na kufanya mambo yote yaanze kusimama?”
“Lakini mama kama kidonda nimekubali kwa nini mniwekee vikwazo kwenye maisha yangu?”
“Si vikwanzo bali masharti ya mizimu.”
“Kama ni masharti ya kunyanyasana mimi siyawezi, kama mali zenu chukueni na mimi niacheni na maisha yangu.”
“Masalu unajiamini nini mwanangu?”
“Sina cha kujiamini bali ukweli ndiyo huo.”
“Basi baba nakuomba, nipo chini ya miguu yako, kama una mwanamke achana naye.”
“Nikueleze mara ngapi kuwa sina?”
“Najua tumekufanyia kitu kibaya lakini mabadiliko ya kidonda chako ni hayohayo.”
Niliachana na mama ambaye niliona na yeye ananizingua, sikutaka kukosa vyote, mavazi nilibadilika kuvaa siku zote nilivaa suruali za kitambaa ili kuogopa kukitonesha kidonda, sikuruhusiwa tena kuvaa viatu zaidi ya sandozi. Kila mmoja alinihoji uwezo wangu wa kifedha na mavazi yangu.
Nilikuwa na duka kubwa kuliko ndugu zangu, lakini wao ndiyo walionekana wana maisha mazuri. Nami sikutaka kushindana nao, kwa vile kidonda nilijua hakitoki mwilini mwangu nami niliamua kutumia kilicho ndani ya uwezo wangu.
Nilianzisha tabia ya kumhonga pesa mpenzi wangu ili naye afaidi kama ndugu zangu kutokana na kuonekana wao ndiyo wenye thamani. Siku moja niliamka asubuhi nyumbani kwangu kama kawaida na kushangazwa kukuta baba yangu na ndugu zangu wakiwa nje ya nyumba yangu.
Eti shida yao kubwa ilikuwa ni kunifumania na mwanamke, niliwashangaa watu wazima kama wale kuacha kazi zao za msingi kutaka kunifumania mimi. Ajabu ya Mungu siku ile mpenzi wangu hakulala nyumbani, sikutaka kupigizana nao kelele. Niliwaruhusu wamtafute, walifanya upekuzi bila kuona lolote.
“Jamani kama bado hamjaridhika semeni niwafungulie wapi mkatafute?”
“Wee chonga lakini lazima utakumbuka siku moja kuwa sisi tulitangulia kuzaliwa.”
“Hilo ni dua la kuku ambalo halitanipa asilani.”
8
Wote waliondoka na kuniacha nikijiuliza kama wangenikuta na mwanamke wangenifanya nini maana walionekana kabisa walikuja kishari.
Baada ya kuondoka niliapa kufanya ninachokiweza, sikuwa tayari kugeuzwa kitega uchumi cha watu. Niliendelea kufanya mapenzi na mpenzi wangu kama kawaida japo hata biashara kwenye duka langu zilidoda, hazikwenda kama mwanzo.
Yote hayo sikuyafikiria zaidi ya kusubiri litakalotokea japo mama alijitahidi kunibembeleza niachane na yote yanayoonekana yanaharibu biashara za familia yetu ikiwemo na yangu. Baada ya kuona maneno yamezidi nilianza kuwa mlevi, kila muda nilikuwa nimelewa kitu kilichozidi kuichanganya familia yangu.
Siku moja nikiwa faragha na mpenzi wangu nilishangaa kuziona sehemu zangu za siri zimeingia ndani, nilishtuka sana. Hali ile ilinifanya nikose raha kwa kuamini zile zilikuwa njama za familia yangu kutaka kuona sifanyi mapenzi na mwanamke.
Katika kumbukumbu zangu, nilikumbuka siku moja kabla ya kutokea kwa tukio lile nilipokuwa na mpenzi wangu kuna kitu alinipaka kilichofanya nihisi kama kuwashwa baada ya kumaliza kufanya mapenzi. Na siku ya pili nilitokewa na tatizo lile, ilibidi nimbane kutaka kujua alinipaka kitu gani.
“Masalu juzi nilikutana na dada yako mkubwa aliniomba nikupake dawa hii, nilikataa lakini alinitishia kuniua. Unajua familia yako imeniandama sana kumbuka kuna wakati nikawa nakukimbia nawe ukaamua kutafuta mwanamke mwingine.
“Kitendo kile kiliniuma sana na kuamua kurudiana na wewe, ndipo juzi nilipokutana na dada yako aliyenipa dawa hii nikupake kabla ya kufanya mapenzi itasaidia kupunguza madhara yanayotokana na matatizo ambayo yangekupata.
“Nilikubali kuipokea kwa vile sikudhania kama dada yako angekufanyia kitu kibaya, kumbe nia yake ilikuwa hii ya kukufanya hivi.”
“Lakini kwa nini amenitenda hivi?” Nilijikuta nikilia kwa uchungu kwa kitendo cha dada yangu.
“Mpenzi sikuwa na nia mbaya, kama ningekuwa na nia mbaya leo ningekuwepo hapa?”
“Ona jinsi ulivyonimaliza, hujui ugomvi wangu na familia yangu umekuwa kama mgeni unakubali kunimaliza, ona sasa,” nilisema kwa uchungu huku nikimuonesha sehemu zangu za siri zilizokuwa zimerudi ndani.
“Nisamehe Masalu sikujua yatatokea yaliyotokea.”
“Wameniweza,” nililalamika kwa uchungu.
Nilijikuta nikiapa kupambana nao, nilipanga sitakwenda tena dukani na nilikuwa nipo tayari kufa kwa njia yoyote ili tu niwaachie maisha yao.
“Masalu kwa nini usiende hospitali kuangalia afya yako kuliko kujikatia tamaa,” mpenzi wangu alinishauri.
“Hospitali haitasaidia kitu wameishaniweza kwa msaada wako, ona tena sina thamani ya uanaume, kimebakia kichwa kama kobe. Haya ni maisha gani ya kukoseshana raha?”
“Kama mambo ya kienyeji twende kuna babu mmoja namfahamu anaweza kazi hii.”
“Unanifikiri atanisaidia nini?”
“We, twende yote tutayajua huko huko.”
Nilikubaliana na mpenzi wangu niende kwa mtaalam aliyekuwa akikaa Pasiansi kuvuka kota za benki. Sikutaka kupoteza muda tuliondoka muda uleule kwenda kwa mtaalam kuangalia kama tatizo langu kama linatatulika. 
Kabla ya kwenda kwa mganga nilitulia ili nitafakari kama nitapata ufumbuzi wa tatizo langu bila kwenda huko. Baada ya sehemu zangu za siri kukosa nguvu nilipata mabadiliko mwilini kwa kidonda kuanza kutoaji maji upya huku biashara nazo zikifunguka.
8
Nilimtolea uvivu dada yangu kwa kumfuata kwenye duka lake na kumshutumu mbele ya wafanyakazi wake kwa kitendo chake cha kishrikina cha kumpa dawa ya kuniua sehemu za siri mpenzi wangu.
Dada alikimbia dukani huku watu wakinishangaa, ugomvi wangu haukuishia pale nilimfuata kwake usiku akiwa na mume wake na kuendelea kumshtumu. Lakini dada alinisihi suala lile tukalizungumze kwa wazazi.
“Masalu utanilaumu bure mpango huo ni wa watu wengi si wangu peke yangu.”
“Kwa hiyo baada ya kunipa kidonda hamkuridhika mmeniua nguvu za kiume?”
“Lakini Masalu si ulielezwa madhara ya wewe kutembea na mwanamke?”
“Kuna madhara gani? Mbona ninyi mna wanaume na watoto au mnataka niwe shoga?”
“Hapana usifanye hivyo.”
“Nakuhakikishieni baada ya kuniua nguvu za kiume sasa natafuta mwanaume wa kufanya naye mapenzi,” nilisema kwa hasira.
“Masalu maneno gani hayo?”
“Tena kawaambie na wanga wenzako.”
“Masalu ukifanya hivyo utatudhalilisha.”
“Heri niwadhalilishe kuliko kunidhalilisha kuna faida gani ya mimi kuitwa mwanaume si bora niolewe?”
“Najua tumekukosea lakini unatakiwa ujue madhara yanayoweza kukupata, tumefanya vile kuokoa maisha yako.”
“Maisha yangu hamuwezi kuyaokoa ninyi si Mungu.”
“Hapana, kutokana na kafara iliyofanywa ya utajiri, ukifanya kosa kama la Monika lazima wewe au baba mmoja wenu atakufa.”
“Wacha nife mimi kwani nina faida gani?”
“Hapana Masalu una faida kubwa kosa lako litagharimu mambo mengi katika familia yetu. Hatukuwa na jinsi imetubidi tufanye hivyo bila hivyo hali ilikuwa mbaya sana, muda wote huo baba alikuwa mgonjwa mahututi alikwishaanza kupooza sehemu moja.
“Amini usiamini kuacha kwako kufanya mapenzi sasa hivi baba ndiyo ameanza kupata nafuu hata chooni anakwenda peke yake. Masalu hebu kuwa na huruma na baba hana nia mbaya sema ni kiburi cha Monika wala kidonda hiki kisingekuja kwako.”
“Ina maana Monika yeye alikuwa hana haja ya maisha mazuri au kuwa na mtoto?”
“Maisha mazuri angeyapata tu, kidonda hiki kina muda wake ukikaa nacho kwa miaka ishirini hupotea na wewe kufanya mambo yako bila kipingamizi, mtoto utapata tu mdogo wangu wala usijigeuze mwanamke.”
“Dada yaani nikae miaka ishirini bila kuwa na mwanamke nina mkataba na Mungu wa kuishi miaka yote hiyo?”
“Masalu usipofanya mapenzi utapungukiwa na nini?”
“Si swali la kuniuliza, kama unaona sipungukiwi na kitu mbona umemhonga mwanaume gari?”
“Masalu sasa hayo maneno gani?”
”Huo ndiyo ukweli wenyewe, kila mwanadamu ameumbwa kufurahia mapenzi pia kupata watoto.”
“Najua ni kweli , lakini kumbuka lililotokea lilihatarisha maisha ya baba, hatukuwa na jinsi.”
“Basi kama hamna jinsi niacheni niishi maisha niyatakayo.”
“Hapana mdogo wangu, hebu punguza munkari tukae kikao cha familia     
ili tutafute ufumbuzi wa tatizo lako.”
“Hakuna ufumbuzi wowote zaidi ya kuniongezea machungu, nakueleza ukweli sikupendi wewe na wote walionizunguka.”
“Masalu utatulaumu bure, kila kitu baba ndiye anayefahamu.”
“Sasa kama anafahamu kwa nini mnanitesa mimi, si mgemuacha akafia mbali.”
“Masalu kuwa na huruma.”
“Niwe vipi na huruma wakati ninyi hamna huruma na mimi, mmemuua dada Monika bila kosa.”
“Masalu Monika kajiua mwenyewe, amekiuka masharti aliyopewa.”
“Muongo mkubwa, nina kila kitu mlichomfanyia, hivi dada kwa Mungu utamwambia nini ikiwa ulimtoa mtoto wako kafara ili upate mali?”
“Nani kakwambia?” Dada alishtuka kusikia vile.
“Nina siri ambazo hata wewe huzijui juu ya familia yetu inayoendekeza ushirikina.”
“Masalu una siri gani?”
“Ya wewe kumtoa mtoto wako ili upate utajiri na kuwekwa ndani ya chumba.”
“Masaluu! Habari hizo umezitoa wapi?”
“Unaweza kuamini kuwa ni siri, kuna siri gani ikiwa dada Monika ndiye aliyekuwa akiipaka mafuta maiti ya mwanao.”
“Wewee!” Dada alizidi kushangaa.
“Kibaya zaidi mmemuua dada Monika mmeshindwa kumzika na kumuweka ndani kama mwanao. Na wewe siku hizi ndiye unayempaka mafuta, hivi kwa mtindo huo kwa Mungu mtasema nini?”
“Masalu nani kakueleza yote hayo au mama?”
“Utamsingizia bure mama kama wewe, ninayo mengi ambayo wewe huyajui.”
”Masalu mambo gani?”
“Siwezi kukueleza muulize baba si ndiye anayefanya yote haya, hata hiki kidonda nilielezwa mapema kitanipata.”
“Na nani?”
“Na dada Monika, hata kifo chake alinieleza kitakavyompata.”
“Alijuaje?”
“Siku alipoondoka baba alimwambia lazima atakufa.”
“Monika muongo.”
“Kweli kabisa na hata alipotaka kufa alinieleza sema siku ya kufa nilikuwa shule kuna siri nzito alitaka kunipa lakini bahati mbaya sikuwepo. Hata mwanaume aliyekuwa akikaa naye hakumpa siri hiyo dada yangu amekufa na siri nzito hata sijui ni siri gani?”
“Wewe unamuamini?”
“Nisimuamini vipi hata bwana’ake mmemuua?”
“Nani kakwambia tumemuua?”
“Najua kila kitu, mimi si mtoto ndiyo maana nimekueleza najua unayoyajua na usiyoyajua.”  
                                                            ******                         
Kila nililokuwa nikimueleza dada aliona kama maluweluwe, niliamua kuondoka huku nikiwa na akili kichwani mwangu.
Wazo la kwenda kwa mganga sikulitupa mbali japo lilikuwa mtihani kwangu. Lakini niliamini maisha yangu yananitegemea mimi mwenyewe si mtu mwingine. Siku ya pili nilimpigia simu mpenzi wangu ili anifuate na anipeleke kwa mtaalamu huyo. Alinifuata na kunipeleka kwa mtaalamu mmoja aliyekuwa maeneo ya Pasiansi nyuma ya kota za benki.
Tulipofika eneo la mganga tulikuta kuna wagonjwa wengi kiasi, ile ilinipa moyo kuwa huduma za mganga ni nzuri. Ilibidi tukae chini ya mti kusubiri wagonjwa wahudumiwe. Baada ya saa tatu ndipo tulipoitwa sisi, ilikuwa ni majira ya saa kumi jioni. Tuliingia ndani na kuketi kwenye mkeka.
“Huyu ni nani?” Mganga aliniuliza.
“Mchumba wangu,” nilimjibu.
“Mbona inaonesha kwenu hawamfahamu?”
“Ni kweli kwetu hawamfahamu.”
“Sasa kama kwenu hafahamiki mizimu haiwezi kuzungumza mbele yake.”
“Kwa hiyo?”
“Akatusubiri nje.”
“Sweet kanisubiri nje,” nilimueleza mpenzi wangu ambaye alionesha hakupenda kutoka nje.
Mpenzi wangu alitoka nje na kuniacha na mganga ndani ya kilinge, baada ya kutoka nje, mganga naye alitoka nje na kurudi na kipande cha tawi la mti wa mnyaa na kuushikilia mkononi. Alipoingia alikaa kwenye mkeka kisha alinipa kipande cha mnyaa ambacho nilishika kwa muda kisha aliniambia nikiachie. Baada ya kukiachia alisogeza karibu na sikio kama anasikiliza simu kisha alianza kuzungumza kama mtu anayezungumza peke yake:
“Masalu mimi jamani mbona kila siku matatizo sifai chini sifai juu, kiuno kinaniuma mgongo unaniuma miguu inaniuma kifua kinaniuma shingo inaniuma kichwa kinaniuma macho hayaoni vizuri choo sipati vizuri, jamani ni kwa sababu gani?
“Masalu mimi nina tatizo gani jamani, mbona kila siku matatizo yanaongezeka ni kweli mganga atanisaidia mbona mimi ni maiti inayotembea ninayesubiri kufa. Ni kweli mganga atanisaidia? Mbona sina thamani ya dunia kifo changu kashikilia baba kama cha dada Monika.
“Maisha haya mpaka lini kidonda mimi na sasa wamechukua nguvu zangu za kiume. Nini kimebakia kama si uhai wangu, kweli mganga atanisaidia?”
Baada ya kusema yale aliondoka kipande cha mti wa mnyaa sikioni na kuutupia kwenye kapu la dawa lililokuwa pembeni yake.
“Umesikia?”
“Ndiyo.”
“Yaliyozungumzwa yana ukweli?”
“Ndiyo.”
“Unajijua kuwa wewe ni maiti?”
“Maiti?” Kauli ya mganga ilinishtua sana.
“Hujijui?”
“Sijijui.”
“Mpaka sasa hivi upo sawa kama nduguzo?”
“Kivipi?”
“Viungo vyako vipo sawa?”
“Vipo sawa.”
“Kipi kilichokuleta hapa?”
“Mambo mengi.”
“Moja wapo?”
“Ni mengi ila kubwa ni hii hali iliyojitokeza hivi karibuni ya kufa nguvu za kiume.”
“Hujui sababu zake?”
“Najua.”
“Sasa nini kimekuleta huku?”
“Mwenzangu alinieleza unaweza kunisaidia.”
“Nikusaidie nini?”
”Kuitoa hali hii?”
“Kidonda umeridhika nacho?”
“Nasikia nikikitoa panaweza kutokea matatizo katika familia yetu.”
“Kama unajua hivyo kwa nini unataka dawa ya nguvu za kiume?”
“Kama utajiri ni wao lakini mapenzi ni haki yangu ya msingi.”
“Sikiliza kijana usijitoe akili,  kwa jinsi alivyokuelekeza dada yako mkubwa juu ya kupona nguvu zako za kiume, nini kitampata baba yako?”
“Kwa hiyo nibaki na hali hii milele?”
“Ni uamuzi wako, kupona upoteze watu au uendelee kuwa maiti inayotembea ili kuiokoa familia yako. Na hiyo mosi familia yako sasa hivi itakutuliza ndani kwa kupooza miguu, utakuwa wa kula na kulala wao wanaponda maisha.”
“Eti?”
“Ukweli ndiyo huo mpango huo utatekelezwa mara moja baada ya kuonekana umekuwa mkaidi.”
“Sikubali.”
“Kama hukubali utafanya nini?”
”Nitatibiwa kila kitu nihakikishe napona na litakalowatokea watajijua wenyewe.”
“Usiseme kwa hasira, upo tayari kuisambaratisha familia yako?”
“Nipo tayari.”
“Kwa kukupa mfano mdogo, dawa utakayokunywa itarudisha nguvu zako za kiume, lakini ukirudi nyumbani utamkuta baba yako yupo hoi kitandani.”
“Kitakachofuata?”
“Siku ukifanya mapenzi ndiyo siku ya kifo chake.”
“Mmh!” Niliguna.
“Ukweli ndiyo huo, chagua kusuka ama kunyoa?”
Nilibakia kimya kwa muda nikiwaza nitakachokifanya na matatizo ambayo yangeikuta familia yangu. Nilikuwa radhi kuendelea na kidonda changu na kukosa nguvu za kiume. Lakini maelezo ya mganga kuwa wanataka kunigeuza msukule kwa ajili ya kuendeleza mali kilinichanganya sana.
Kufikia pale nilijikuta nikichanganyikiwa na kushindwa niegemee upande gani, lakini niliamini maisha yangu ni muhimu kuliko kitu chochote chini ya jua. Vilevile  sikuwa tayari kumhurumia mtu aliyepanga kuniangamiza kwa ajili ya tamaa zake za mali.
Uamuzi nilioamua ni kujitengeneza mimi na lolote litakalotokea kila mmoja ataubeba msalaba wake.
Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu mganga alinishtua.
“Vipi umeamua nini maana naona umekaa kimya?”
“Mzee wangu mambo ni mazito kila ninalofikiria naliona zito.”
“Kwa hiyo tuache kama ilivyo?”
“Mzee wangu huna ufumbuzi mwingine usio na madhara?”
“Sikiliza kijana wewe unajua matatizo ya familia yenu kuliko mimi, hebu nisaidie nifanye nini?”
“Wewe si ndiye mtaalamu ninayekutegemea?”
“Hutaki kunisikiliza, kwani mimi napenda kuona matatizo, lakini mambo yenyewe yamekaa vibaya.”
“Kwa hiyo?”
“Nimekueleza yote una uamuzi wako mwenyewe wala siwezi kukuingilia lakini ukweli ndiyo huo.”
“Basi fanya unavyoweza.”
“Vipi?”
“Utakaloliona linafaa.”
“Kijana acha kujitoa akili, mimi sipo hapa kwa ajili ya kuwachagulia wateja jinsi ya kufanya.”
“Mzee wangu kwa vile mpango wao ni mbaya kwangu naomba unisaidie mimi.”
“Kwa hiyo upo tayari kwa lolote litakalotokea?”
“Nipo tayari.”
Leo nitaanza kukupa dawa ya kurudisha nguvu za kiume, lakini usishtuke kusikia taarifa zitakazokufikia ambazo zitajenga uadui mkubwa kati yako na nduguzo.”
“Siwezi kushtuka kwa viumbe wasio na huruma na mimi, wewe nipe hiyo dawa kila mtu ataubeba mzigo wake mwenyewe.”
“Haya nisubiri.”
Mganga alinyanyuka na kutoka nje, akiniacha na uamuzi mmoja ambao nilikuwa tayari kwa lolote. Baada ya muda aliniita nje, nilitoka na kuelezwa nisubiri kwenye kigoda. Baada ya muda nilimuona mpenzi wangu akiwa amebeba ndoo kutoka kwenye kisima kilichokuwa pembeni ya nyumba ya mganga.
Alipofika, mganga alimueleza ayapeleke nyuma ya nyumba na kuyaweka kwenye beseni. Alifanya vile, aliporudi mganga alizunguka nyuma na baada ya muda aliniita. Nilimfuata na kukuta kuna beseni lililokuwa na maji yaliyochanganywa na dawa ya unga na majani mabichi kama ya mnyonyo.
“Oga haya maji, kisha haya majani utajisugua sehemu zako zisizofanya kazi, sawa?”
“Sawa.”
“Haya, ukimaliza kuoga vitu vyote viache hukuhuku.”
“Hakuna tatizo mzee.”
Mganga aliondoka na kuniacha nikivua nguo na kuanza kujimwagia maji kwa mikono huku nikijisugua kwa majani yale mabichi sehemu zangu za siri zilizokwisha nguvu. Baada ya kumaliza kuoga nilirudi kwa mganga, alinielekeza nikae kwenye kigoda kisha alizunguka nyuma ya nyumba, sikujua anakwenda kufanya nini, mara alirudi akiwa ameshikilia majani niliyojisugulia na kuingia kwenye kilinge chake. Baada ya muda aliniita.
Niliingia kibandani na kuketi kwenye ngozi ya ng’ombe, baada ya kuketi mganga alinipa maji yaliyokuwa kwenye kikombe cha plastiki. Nilikunywa maji yale kisha nilimrudishia kikombe, baada ya kukipokea alisema:
“Sasa nafikiri kazi tumemaliza, weka hapo kwenye kikapu kiasi chochote kama sadaka kwa mizimu.”
Nilichomoa pochi na kuweka elfu hamsini, baada ya kuweka mganga alisema:
“Mpaka sasa kwenu kuna hali ya sintofahamu, inaonesha hapa baba yako ameanguka dukani na anarudishwa nyumba. Ukitaka kumuua haraka baba yako ukikutana na mpenzi wako haimkopeshi, salamu utasikia.”
“Sasa mganga kama ni hivyo kuna faida gani ya kuja kwako?”
“Nilikuwa nakujulisha tu, litakalotokea usishangae, kesho asubuhi njoo haraka maana kuna vita nzito itakayotokea. Itakuwa mara mbili ya leo, ningeweza kukutengenezea zindiko lakini siwezi kufanya kazi mbili kubwa kwa wakati mmoja.”
“Hakuna tatizo.”
“Basi wewe nenda nyumbani, kama unaweza usionane nao watakutafuta sana ili kuhakikisha baba yenu anarudi katika hali ya kawaida. Na kurudi kwa afya ya baba yako, huchukui muda unakuwa msukule wa familia wa kuwaingizia pesa.”
“Siwezi kukubali, kama nimepona nitaendelea na mpenzi wangu kwa vile bila yeye nisingeweza kupona.”
“Pia kuna kitu cha ajabu kitamtokea baba yake, sumu ya uchawi itamgeuza kiumbe cha kutisha.”
“Vyovyote atakavyokuwa mimi hainihusu, yule sasa ni adui yangu na si mzazi wangu,” pamoja na maneno yale kuwa ya kutisha sikuingiwa huruma kwa vile wao walitafuta uhai wangu.
“Hiyo ni juu yako kwa vile yote nimekueleza bila kuacha kitu.”
                                                       *****
Baada ya maelezo ya mganga, nilitoka na kumpitia mpenzi wangu na kuondoka, tulipofika Pasiansi tulitafuta sehemu kupata chakula kutokana na njaa iliyokuwa ikituchonyota.
Wakati wa kula nilijikuta mtu mwenye mawazo mengi, kitu kilichomshtua mpenzi wangu na kutaka kujua kulikoni.
“Masalu kuna nini mbona unaoneka una mawazo mengi?”
“Ni kweli, nina mtihani mzito.”
“Upi huo?”
“Kuhusiana na hali yangu, kama nilivyokueleza, kuna mambo mazito yamejitokeza.”
Sikuwa na jinsi nilimueleza kila kitu, sikutaka kumficha kwa vile msaada wake ndiyo uliofichua yote. Baada ya kunisikiliza alishtuka sana.
“He!”
“Ndiyo hivyo nikubali ili nigeuzwe ndondocha au niokoe maisha ya baba  na familia kukutwa na matatizo mazito.”
“Mmh! Huo mtihani, lakini maisha yako ni muhimu kuliko kitu chochote.”
“Nami ndiyo nimefanya hivyo, ila mganga ameniomba leo nisionane nao ili kesho turudi mapema kwake.”
“Hakuna haja ya kuhangaika, tutafute gesti yoyote nzuri hapahapa Pasiansi ili kesho turudi kwa mganga mapema.”
“Kweli wazo zuri, basi tufanye hivyo.”
Nilikubaliana na mpenzi, wangu baada ya chakula tulitafuta nyumba ya wageni yenye hadhi na kupanga pale.
Siku ile tulishinda na kulala pale, majira ya saa tano za usiku dada alinipigia simu, nilitaka kuacha kuipokea lakini niliamua kuipokea.
“Haloo.”
“Haloo Masalu.”
“Shikamoo”
“Marahaba.”
“Unasemaje?”
“Masalu upo wapi?”
“Una shinda gani?”
“Masalu umefanya nini?”
“Kuhusu nini?”
“Unataka kumuua baba?”
“Kumuua kivipi?”
“Masalu baba akifa utamla nyama.”
“Kama mlivyo mla nyama dada Monika?”
“Nini?”
“Umenisikia vizuri.”
“Wee fanya mzaha, lakini ole wako baba afe.”
“Na wewe ole wako siku ukisogeza pua yako kwangu utanitambua mimi ni nani mwanga mkubwa we, kwanza nilikuwa nakuchekea sasa hivi sikupendi nakuchukia ni adui yangu namba moja na taarifa zako nazipeleka polisi.”
“Polisi! Utawaambia nini?”
“Kwamba wewe na wenzako ni wauaji.”
“Tumemuua nani?”
“Dada Monika na mtoto wako na ushahidi wa sehemu ulipoziweka hizo maiti ninao na lazima mtanyongwa mwaka huu.”
“Masalu usifike huko hali ya baba ni mbaya sana, hebu rudi nyumbani tujue tufanye nini,” ilibidi arudishe sauti chini.
“Nirudi mnimalize.”
“Tukumalize?” Alijifanya kushtuka.
“Eeh, baada ya kuniua nguvu za kiume sasa mnataka kunigeuza msukule.”
“Ha! Masalu nani kakudanyanya hivyo?”
“Dada hakuna siri duniani, yaani pamoja na kunipa kidonda hamkuridhika pamoja na utajiri na maisha mazuri kupitia mwili wangu. Mkaamua kuniua nguvu za kiume ili nisiwe na thamani yoyote dunia. Haitoshi mmeniandalia pigo zito la kunimaliza kabisa la kunigeuza msukule ili tu muwe na maisha mazuri.
“Ninyi ni viumbe gani mnaojali fedha kuliko utu wa mtu, mmemtoa kafara dada Monika kwa tamaa zenu, hamkuridhika umemtoa mtoto wako ili uwe na pesa nyingi vile vile hamkuridhika mmenigeukia mimi. Kwa vile hakuna mtu mwingine wa kumpa kidonda hiki mmeamua mnigeuze ndondocha wa familia.”
“Masalu umejuaje?”
“Si kujuaje, kwa nini umeamua kunifanya hivyo?”
“Si kweli,” dada alijifanya kushtuka.
“Sawa si kweli, basi baba anakufa.”
“Umeamua kuuana?”
“Masalu bila wewe baba atakufa, unakubali baba yetu afe kweli?”
“Mimi na ninyi nani kaamua kumuua mwenzake?”
“Masalu kumbuka baba yetu ni huyuhuyu, akifa hatutampata mwingine.”
“Kwani kuna mbadala wa dada Monika, baba ni huyo huyo, dada Monika mwingine yupo wapi?”
“Masalu makosa yamekwisha fanyika rudisha moyo uokoe maisha ya baba.”
“Kwanza mnaniambia hivyo mimi nimemfanya nini baba?” niliwauliza swali gumu.
“Inaonekana umekwenda kwa mganga kurudisha nguvu zako za kiume.”
“Mlitaka niwe hivihivi milele kwa raha zenu, mbona ninyi mna watoto na wanaume?”
“Kwani Masalu upo wapi?”
“Tokea lini mlinitafuta?”
“Basi zungumza na mama,” baada ya muda nilimsikia mama akiniita.
“Masalu.”
“Naam mama, shikamoo.”
“Marahaba mwanangu upo wapi? hali ya baba yako ni mbaya sana.”
“Anaumwa nini?”
“Ameanguka kwenye mishughuliko yake, kama ni kweli umefanya wewe njoo umsaidie baba yako, hali inatisha hajitambui anakoroma tu.”
“Mama sihusiani na lolote kuhusiana na matatizo ya baba, naomba mumpeleke hospitali.”
“Ugonjwa huu si wa hospitali.”
“Kwa hiyo mimi ndiye niliyemroga?”
“Hapana Masalu, ila inawezekana ulichokifanya ndicho kilichomuathiri baba yako.”
“Kipi hicho?”
“Unakijua Masalu, hebu rudi haraka nyumbani.”
“Mama ni nani kwako?”
“Mtoto.”
“Nina haki gani kama mmoja wa watoto wako?”
“Haki zote kama walizonazo wenzako.”
“Sasa kama kila mtu ana haki hiyo kwa nini unataka kushiriki katika kunigeuza ndondocha wa familia?”
“Masalu! Wakugeuze kivipi?” mama alishtuka.
“Mama, unajua vizuri sana si suala la siri, mpango wenu wa kunimaliza nimeugundua lakini nawahakikishia kila atakayenigusa nitampoteza.”
“Upo tayari baba yako afe?”
“Mimi situnzi uhai wake bali Mungu aliyetuumba wote, kama wakati wake umefika basi atakufa, kama alivyokufa mtoto wa dada na dada Monika.”
“Kwa nini umekosa huruma?”
“Kwa vile ninyi mnanionea huruma eeeh.”
“Kama ulivyosikia hali ya baba yako ni mbaya kifo chake kitakuhusu.”
“Sishangai hata wewe mama niliyekuwa nakutegemea ni mmoja wapo. Asante sana nashukuru, Mungu yupo atanilinda.”
“Masalu...Masa..,” nilikata simu na kuizima kabisa.
                                                   ******
Baada ya mazungumzo nilijikuta nikilia peke yangu jinsi familia yangu ilivyokuwa ikijijali yenyewe na kuwa tayari kupoteza uhai wa mtu ili tu ipate mali.
“Masalu nyamaza mpenzi wangu,” mpenzi wangu alinibembeleza, kipindi kile yeye ndiye aliyekuwa mfariji wangu.
“Inaniuma.”
“Kweli inauma, lakini kwa nini umekubali kuzungumza nao? Ungezima simu yote haya yasingetokea.”
“Ilikuwa lazima nizungumze nao ili wajue kuwa naelewa kila kitu, pia hata kujua kama kweli hali ya baba ikoje.”
“Kwa hiyo utakwenda kumuona baba yako?”
“Nikitoka kwa mganga nitakwenda.”
“Pole sana inasikitisha, familia yako ina dhambi kubwa.”
“Wee waache sijui kwa Mungu watasema nini?”
“Ulisema wewe ndiye chanzo cha utajiri kilichoachwa na marehemu dada yako Monika, ukipona itakuwaje?”
“Sijui, watajua wenyewe, mimi nitaangalia afya yangu.”
“Mmh! Pole sana mpenzi wangu, kupona lazima uwe na roho ngumu ili umeze mfupa.”
“Nimekwisha umeza lolote na liwe, siwapendi mashetani wale.”
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda tulipanda kitandani kulala, usiku nilijikuta nikipatwa na hamu ya mapenzi. Lakini nilikumbuka kauli ya mganga kuwa nikikutana kimwili na mwenzangu ndiyo kifo cha baba, hawezi kuomba hata maji.
Pamoja na hasira kutokana na roho mbaya ya familia yangu juu ya mambo waliyotaka kunifanyia nilijikuta nikiingiwa na imani ya kutofanya tendo lile kuokoa maisha ya baba. Tulilala mpaka asubuhi bila kufanya tendo la ndoa, asubuhi tuliamkia kwa mganga.
Hatukuchelewa kufika kwa vile hapakuwa  mbali kutoka tulipokuwa tumepanga, ulikuwa mwendo wa dakika ishrini. Ilionesha sisi ndiyo tulikuwa wateja wa kwanza toka nje kufika pale kwa siku ile, tuliowakuta pale ni wale waliokuwa wakitibiwa na kulala palepale.
Mganga alitukaribisha, kama kawaida niliingia ndani peke yangu na mpenzi wangu alibakia nje. Nilipofika hakunisemesha lolote, aliendelea na kutoa chupa za dawa kwenye kikapu na kuziweka juu ya ngozi kisha alichukua karatasi ya kaki na kuanza kumiminia unga wa dawa kidogo kidogo kutoka katika kila chupa.
Zilikuwa chupa zaidi ya tano, baada ya kuukusanya unga wa dawa katika karatasi moja, alichukua chupa iliyokuwa na mafuta kama sikosei ya ng’ombe, yalikuwa meupe na mazito. Aliyamiminia yale mafuta na kuyachanganya na mchanganyiko wa dawa kisha alitoka nje.
Baada ya muda alirudi na kunionesha kwa ishara nimfuate, nilimfuata mpaka kwenye kichuguu kimoja ambacho alinielekeza. Kabla ya kupanda juu ya kichuguu alinielekeza kwa ishara nivue shati. Nami nilifanya kama alivyonielekeza.
Baada ya kupanda juu ya kichuguu kifua wazi, alipanda na yeye na kuanza kunichanja kila kona ya mwili huku akinipaka ile dawa aliyochanganya na mafuta mazito. Alipomaliza tuliteremka na kurudi hadi ndani ya kilinge, ndipo aliponisemesha.
”Habari za toka jana?”
“Nzuri mzee wangu, shikamoo.”
“Marahaba, kuna habari gani mpya?”
“Jana walinipigia simu usiku na kuniomba ninusuru maisha ya baba.”
“Uliwajibu nini?”
“Niliwaambia siwezi kujiteketeza mwenyewe.”
“Wao walisemaje?”
“Walinitishia kama baba akifa nitamla nyama.”
“Akawajibu nini?”
“Niliwaeleza kama walivyokula nyama ya dada Monika.”
“Wakasemaje?”
“Walishtuka na kunieleza kuwa habari nimezijulia wapi?”
“Mh, ukawajibu nini?”
“Niliwambia nitawapeleka polisi na kuwafungulia mashtaka ya uuaji na kukaa na maiti za watu ndani?”
“Enhee! Wakasemaje?”
“Walishtuka na kuniomba ninusuru maisha ya baba.”
“Ukawajibu nini?”
“Niliwaeleza sipo tayari.”
”Wakasemaje?”
“Waliendelea kunibembeleza niende kwa vile uliniahidi nikitoka hapa nitakuwa kamili, nimewaeleza nitakwenda leo.”
“Wakasemaje?”
“Tumekubaliana, nikitoka hapa niende.”
“Sikiliza, una bahati kama usingekuja hapa na kujipendekeza jana ukaenda ungekwisha palepale.”
“He!” Nilishtuka kusikia vile.
“Unashtuka, kama nilivyokueleza familia yako haina mapenzi na wewe kwa ajili ya mali.”
“Mmh! Sasa nikienda leo itakuwaje?”
“Leo usiende, nenda keshokutwa ila kuna kitu kitatokea si cha kawaida, kuwa tayari kukabiliana nacho.”
“Kitu gani hicho?”
“Wee nenda, ila majibu utayapata kujua kinga niliyokukinga inafanya kazi kiasi gani.”
“Niambie ili nijue ikiwezekana nisiende.”
“Lazima uende ili kuwaumbua wabaya wako.”
“Mmh! Sawa.”
“Baada ya kesho kwenda rudi tumalizie tiba, kwa vile hawatakubali kuona umewashinda.”
“Sawa nimekuelewa.”
“Nilitaka kusahau kitu kimoja, leo usioge wala kukutana na mwanamke kimwili ikiwezekana leo kila mmoja alale chumba chake au kitanda chake.”
“Sawa nimekuelewa.”
“Ndoto utakayoiota ndilo jibu la safari yako.”
“Nashukuru kwa msaada wako.”
                                              ******
Baada ya mazungumzo, tulirudi hoteli tuliyokuwa tumepanga kwa ajili ya mapumziko, siku ile sikukaa kutokana na kuwa na alama nyeusi za kuchanjwa na mganga.
Kwa vile hatukuruhusiwa kulala pamoja, tulichukua chumba cha vitanda viwili na kila mtu alilala kitanda chake. Usiku niliota ndoto nafukuzwa na kichaa mmoja ambaye katika kunifukuza aligongwa na gari, hapohapo nilishtuka usingizini na kujiuliza kichaa yule ni nani na ndoto ile inaashiria kitu gani.
Siku ya pili nilimueleza mpenzi wangu ambaye alinishauri heri nisiende nyumbani ili kuepusha nilichokiota.
“Masalu kama mganga alikuambia utakachokiota ndicho kitakachotokea, kwa nini uende?”
“Hilo wazo hata mimi nilikuwa nalo lakini mganga alisema lazima niende, ili nirudi na kupata dawa ya mwisho.”
“Kwa nini asikupe hiyo dawa?”
“Alisema lazima niende ili kuonesha uwezo wa kile alichokifanya jana.”
“Mmh! Mtihani mzito kweli.”
“Lakini kwetu hatuna kichaa.”
“Basi inawezekana utakutana naye njiani.”
“Kama ni hivyo bora nikodi gari mpaka mlangoni.”
“Bora ufanye hivyo.”
“Sawa, basi tuongozane, wewe uende kwenu najua wamekutafuta sana.”
“Hata wakinitafuta mimi mtu mzima, kuna mdogo wangu anajua kila kitu sidhani kama watasumbuka sana. Mbona tuliishasafiri zaidi ya wiki hakuna kilichoharibika?”
“Si uliaga?”
“Basi taarifa zangu watazipata kwa mdogo wangu na leo nikifika watapata jibu.”
“Mmh! Haya.”
Niliongozana na mpenzi wangu hadi kwao, nilimteresha na mimi kuendelea na safari yangu. Nilikwenda na gari hadi mlangoni na kuteremka, wote waliokuwepo walishtuka. Baba aliyekuwa amelazwa sebuleni aliponiona alipiga kelele.
“Mtoeni...mtoeni  ataniua...ataniua.”
“Baba siwezi kukuua, utajiua mwenyewe,” nilimjibu baba.
“Jamani mtoeni ataniua,” baba alizidi kupiga kelele.
“Masalu hebu toka nje,” dada alinifokea.
Niligeuka kutoka nje, kaka yangu alikuja kwa nyuma na kunishika kisogoni, mara alianza kupiga kelele kama mtu aliyepagawa, akachukua jembe na kutaka kunipiga nalo, alinikosakosa mara mbili, nilipoona hatanii nilitimua mbio, alinikimbiza mpaka barabarani huku akidhamiria kuniumiza.
Ilinibidi nivuke barabara bila kuangalia baada ya kuona nakufa najiona, baada ya kuvuka nilisikia kishindo nyuma yangu na kelele za watu. Nilipogeuka nilimuona kaka yangu akiwa chini akivuja damu kichwani.
Japo ajali ile ilifanya moyo uume na kupatwa na huruma, lakini sikutaka kurudi kuangalia, wakati huo watu walikuwa wakijaa kwenye tukio la ajali na kumzunguka kaka. Nilikodi teksi iliyokuwa ikipita kuwahi nyumbani. Nilipofika nyumbani nilimpigia simu mpenzi wangu.
“Vipi Masalu mbona kama kuna tatizo?”
“Ndiyo.”
“Tatizo gani?”
“Si la kulizungumzia kwenye simu.”
“Upo wapi?”
“Nyumbani.”
“Nakuja sasa hivi.”
Baada ya kukata simu nilibaki nimejilaza kwenye kochi nilijiuliza vita nzito niliyoelezwa na mganga ndani ya familia yangu nini hatima yake. Nilijiuliza kaka yangu bila kugongwa na gari alitaka kunifanya nini. Au alikusudia kuniua?
Njozi ile baada ya kuuona ukweli nilijuliza nini kitafuata.
Niliamini kama vita ya nguvu za giza itashindikana basi watatumia nguvu za kawaida ili kunitokomeza duniani. Nilijiuliza kama itakuwa hivyo nitawezaje kuwaepuka? Nilipanga kuukimbia Mji wa Mwanza ili kuokoa maisha yangu kwa kuliuza duka langu.
Wazo lile nilitaka nishauriane na mwenzangu kabla ya kutoa uamuzi, nilipanga akija nitamgusia suala lile ambalo kwa upande wangu lilichukua sura mpya ya kutishia maisha yangu. Wakati nikiwa kwenye dimbwi la mawazo mpenzi wangu aliingia kwa hali aliyonikuta nayo ya kujilaza mikono kichwani ilimshtua sana.
“Vipi?”
“Masalu?”
“Mambo mazito.”
“Kivipi?”
Nilimueleza niliyokutana nayo nyumbani, alibakia mdomo wazi asiamini nilichomueleza.
“Sasa bila kugongwa na gari ingekuwaje?”
“Hata sijui.”
“Sasa kwa nini mganga hakukuambia?”
“Aniambie nini wakati aliniambia nitakayoyaota ndotoni ndiyo nitakutana nayo?”
“Sawa, lakini alitakiwa akupe tahadhari.”
“Mganga hawezi kukuambia kitu kijacho kabla ya kutokea ili usije sema uongo.”
“Pole sana mpenzi wangu sasa tutafanya nini?”
Mara simu yangu iliita nilipoangalia nilikuta ni dada, niliitazama bila kupokea kitu kilichomfanya mpenzi wangu kuuliza.
“Mbona hupokei ni nani?”
“Dada”
“Anataka nini si alikufukuza?”
“Hata mimi nashangaa.”
“Usipokee.”
Kweli sikuipokea, iliita mpaka ikakatika, baada ya kukatika haukupita muda iliita tena. Vilevile sikuipokea, ikaita mpaka ikakatika. Nilitaka kuizima lakini mpenzi wangu alikataa kwa kuniambia:
“Simu za ndugu zako usipokee, lakini zingine ziache ziingie.”
“Kutokana na vita hii nzito nilikuwa nimepanga kuuza duka langu niondoke Mwanza, ulikuwa na wazo gani?”
“Mmh! Ni haraka sana kwa nini tusirudi kwa mganga tumsikilize atasema nini?”
“Mganga kazi yake ni kunizindika ili nisidhurike na nguvu za wachawi, lakini si kuwazuia kunidhuru kwa silaha za kawaida.”
“Sawa, lakini kabla ya kufanya hayo tukamsikilize mganga, si alikuambia urudi.”
“Mmh! Kweli, kuna umuhimu wa kwenda muda huu.”
“Hakuna tatizo ni muda mzuri.”
Nilikubaliana na mwenzangu kurudi kwa mganga, tuliongozana hadi kwa mganga, tulimkuta akihudumia wagonjwa. Ilitupasa kusuburi kwa zaidi ya saa nne. Ilipofika zamu yangu niliingia kwa mganga, aliponiona alitabasamu na kusema:
“Umeona?”
“Ndiyo.”
“Sasa ule ndiyo ubaya uliokuwa umekuzunguka, bila kupitia hapa alipokushika ungeanguka chini na kupooza, kuanzia muda ule ungewekwa kwenye chumba chenye mwanga hafifu na hayo ndiyo yangekuwa maisha yako mpaka unakufa.”
“Mmh! Na kaka yangu aliyegongwa na gari hakufa?”
“Hakufa.”
“Atapona?”
“Atapona, lakini itachukua muda mrefu sana kupona, alipogongwa hakuumia. Lile halikuwa gari la ukweli kama ulivyodhania ni kinga yako mwilini hakuna wa kukuchezea. Atakayetaka kukuchezea atapatwa na mazito kuliko yaliyompata kaka yako.
“Kila tatizo litakalokutokea utaliota usingizini kabla ya kukutokea.”
“Kwa hilo nashukuru, lakini wakitumia silaha?”
“Zindiko nililokuwekea hawawezi kukudhuru kwa kitu chochote.”
“Nilikuwa na wazo la kuuza duka ili nitoroke.”
“Wala usiende popote, hakuna wa kukugusa, watakuogopa kama ukoma, ila inabidi duka lako lifanyiwe zindiko bila hivyo mali zako zote zitamomonyoka na kukufanya ubaki kuwa maskini wa kutupwa.”
“Na ndugu zangu?”
“Nao wana wakati mgumu, si muda mrefu watakuwa na maisha magumu, labda wahangaike tena la sivyo kwa kutegemea ndagu ya kidonda wataadhirika.”
“Kwa hiyo unataka kuniambia kaka hakupata ajali?”
“Hakupata ajali ila amepata kichaa baada ya kutaka kukudhuru na kumrudia mwenyewe.”
“Lile gari na watu waliokuja walitokea wapi?”
Kile ni kiini macho tu lakini ile ndiyo kinga inayokulinda, baada ya kumzuia ulipata nafasi ya kukimbia na kurudi kwako.”
“Na hali ya baba?”
“Mmh! Hali ya baba yako ndiyo hivyo imeshikiliwa na uhai wako, kubali uteseke baba yako apone.”
“Sipo tayari wacha afe, siwezi kuwaonea huruma tena ni watu wabaya wasionitakia mema.”
“Basi leo nitamalizia kazi yangu, ukitoka hapa fanya mambo yako bila hofu, atakayekugusa atapotea.”
Mganga baada ya kusema vile alichukua dawa nyeusi iliyokuwa kwenye chupa na kuichanganya na asali kisha alisema niachame mdomo, akanichanja kwenye ulimi na kunipaka dawa kwa kutumia simbi. Chale zingine alinichanja katikati ya utosi, kifuani na mgongoni na sehemu zote za maungio ya mwili kisha alinipa ruhusa ya kurudi nyumbani na kunipa masharti yaleyale ya kutolala na mwanamke kwa siku ile.
“Kijana kazi imekwisha, unaweza kuendelea na shughuli zako kama kawaida.”
“Asante, na kuhusu hali ya baba?”
“Yangu nimemaliza, utaamua mwenyewe.”
“Hawezi kupona tena?”
“Akipona ujue unakufa wewe.”
“Hata akipelekwa kwa mtaalamu mwingine?”
“Kwangu nimemaliza na kazi yangu naiamini haijawahi kutokea kama itatokea basi ujue ndiyo kifo chako.”
“Na asipopona?”
“Utakufa.”
“Sasa itakuwaje, ndugu si watajua mimi ndiye niliyemuua?”
“Kijana niondolee upumbavu, niambie unataka nifanye nini, ufe baba yako apone au afe baba yako wewe upone?” Mganga alikasirishwa na maswali yangu.
“Basi mzee nisamehe,” niliomba msamaha baada ya kuona nimemuudhi mganga.
“Sjawahi kuona mtu mpumbavu kama wewe, unanipotezea wakati wangu nakuomba uondoke,” mganga alikuja juu na kunifukuza.
“Samahani mzee wangu,” nilijikuta nikichanganyikiwa baada ya kumuudhi mamba kabla sijavuka mto.
“Samahani nini, nilikuita hapa nikutibu?”
“Hapana.”
“Nilikuomba nikusaidie?”
“Hapana.”
“Sasa kwa nini unanitia ujinga kwa kazi nzito niliyoifanya ya kuokoa maisha yako?”
“Nisamehe mzee wangu nipo chini ya miguu yako sitakuuliza tena swali lolote kuhusiana na familia yangu.”
“Kazi nimemaliza nipe changu kilichobaki kisha uende zako utaamua chochote kwenda kwa mganga yeyote akusaidie. Ila ukiondoa mguu wako hapa usije tena.”
“Mzee wangu najua nimekukosea naomba usifike huko,” nilizidi kumuomba msamaha mganga baada ya kubaini kosa langu.
“Lazima nifike nimekufafanulia mangapi yaliyotaka kukupata na leo umepata jibu bado unajitoa akili nikufanye nini? Wewe mtoto?”
“Hapana, nimekosa mzee wangu nipe adhabu yoyoye lakini usinikataze kuja hapa,” nilipiga magoti mbele ya mganga kuomba msamaha.
“Nimekuelewa kijana lakini usirudie tena kuingilia kazi za watu.”
“Nashukuru mzee wangu.”
                                                   ******
Baada ya kusamehewa na mganga, tuliagana na kunieleza ninapotokewa na tatizo niende kwake bila tatizo.  Baada ya kutoka pale sikutaka kurudi nyumbani ambako niliamini lazima ndugu zangu watanitafuta.
Kama  kawaida tulirudi kwenye hoteli yetu tuliyolala jana yake, tulilala pale mpaka siku ya pili. Usiku wa siku ile mpenzi wangu alitaka kujua nini hatima ya maisha yangu baada ya kutoka kwa mganga.
“Mh, Masalu mganga amesemaje juu ya uamuzi wako wa kukimbia mji?”
“Amesema hakuna kitakachonitokea nikae hapahapa.”
“Na kuhusu ile ajali?”
“Anasema haikuwa ajali bali kinga aliyoniwekea ndiyo iliyonilinda nisidhuliwe na kaka.”
“Masalu! Unataka kuniambia kaka yako hakugongwa na gari?”
“Mganga ndivyo alivyonieleza.”
“Mmh! Makubwa, lakini mganga huyu kiboko, sifa zake ni kubwa.”
“Lakini alitaka kunitimua.”
“He! Kivipi?”
“Nilitaka kumuulizia hatima ya hali ya baba yangu.”
“Akakujibu nini?”
“Wewe, kumbe niliwasha moto wacha anifukuze kama mbwa aliyeiba mayai.”
“Ehe! Ikawaje?”
“Mmh! Ilibidi nimuombe msamaha huku ninalia.”
“Mkaishiaje?”
“Alinisamehe na kunionya nisirudie tena kuuliza maswali ya kijinga.”
“Lakini nawe umeyataka, unamuombea dhamana mtu uliyemfunga mwenyewe?”
“Pamoja na hayo, lakini yule ni mzazi wangu.”
“Haya sasa, chagua mzazi apone uumie wewe.”
“Japo inaniuma lakini kisu kimegusa mfupa, kungekuwa na njia mbadala nisingekubali kuona baba yangu anateseka kwa ajili yangu.”
“Lakini ningekuwa ni mimi nisingekuwa na huruma na mtu anayenitoa kafara kwa tamaa zake. Tena ningemuulia mbali hata kwa sumu.”
“Lakini kumbuka pamoja na yote ni mzazi wako.”
“Siwezi kumuonea huruma mzazi mwenye nia mbaya na mimi, akitaka kuniua nikigundua na mimi namfanyia kitu kibaya.”
“Lakini si kila baya lazima ulipe baya kuna lingine  unatakiwa kulisamehe.”
“Kwa upande wako utasamehe vipi, ili kupona lazima mtu aumie, kibaya zaidi pamoja na yote waliyokufanyia bado wanataka kukupoteza kwenye sura ya dunia bado watu kama hao unawaonea huruma?”
“Kwa kweli nimechanganyikiwa.”
“Sikiliza Masalu, unapofanya kitu kibaya kisha ukaona huruma basi lazima litakurudia na halitapata tiba mpaka unakufa.”
“Wewe nani kakwambia?”
“Masalu mpaka nakupeleka kwa yule mganga  nayajua mengi kwa hiyo jiepushe kukingia kifua unayoyafanya, bora ungeacha kabisa kuliko kuingilia kazi ya mganga hasa wakikusaidia katika matatizo yako.”
“Kwa hiyo nikiendelea kusikitika itakuwaje?”
“Usishangae ugonjwa wa baba yako ukakurudia.”
“Lakini sasa hivi si nimeachana nao.”
“Basi ndiyo hivyo, siku zote usioneshe huruma pale unapoamua kutenda jambo zito, huruma yako hugeuka sumu na kukurudia mwenyewe.”
“Nimekuelewa.”
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda tulikubaliana tulale ili mengine tuzungumze kesho yake kwa vile bado tulipanga kuendelea kuwa pale  kwa siku moja zaidi. Kila mtu alilala kitanda chake kama tulivyoelezwa na mganga, ilionesha wazi kabisa mpenzi wangu alikuwa akiumia kutokana na kumnyima haki yake ya msingi.
Lakini bado sikuwa tayari kumuua baba yangu kwa kulifanya tendo lile, hata hali aliyokuwa nayo ilitokana na kuyaokoa maisha yangu yaliyofikia hatua mbaya. Pia hakukuwa na njia mbadala ya kuweza mimi kupona bila baba yangu kuguswa.
Japo mpenzi wangu alionekana hana huruma na familia yangu na kuwa tayari kuiona inapotea baada ya kugundua walikuwa na mpango mbaya kwangu lakini nilijitahidi kutafuta njia ya kumueleza kwa makini ili anielewe, sikupenda hata siku moja kifo cha baba yangu kitokane na mimi kwa kufanya tendo la ndoa nikijua kabisa ndilo litakalomaliza uhai wake.
Pamoja na kujua ubaya wao kwangu, bado sikutakiwa kuua nikijua kabisa chanzo cha kifo kinatokana na nini. Tulilala kila mtu na kitanda chake kwa kuzima taa. Katikati ya usiku niliota ndoto moja baba amegeuka kiumbe cha ajabu chenye manyoya na meno marefu. Nilimuona mama na ndugu zangu wakilia. Kilichonishangaza zaidi alionekana kama kiumbe kisicho na uhai.
Nilishtuka usingizini na kukaa kitako huku nikijiuliza ndoto ile ina maana gani, Nilijikuta nikishindwa kuelewa ndoto ile ina maana gani na kwa nini baba ageuke kiumbe cha ajabu chenye kutisha? Sauti za kilio nilizozisikia  ilionesha wazi msiba ule ni wa baba. Niliamini ndoto ile iliashilia kifo cha baba lakini kubadilika kwa umbile la ajabu lilikuwa likiashiria nini?
Lakini sikutaka kuamini moja kwa moja kutokana na kauli ya mganga kuwa baba yangu atakufa kama nikikutana kimwili na mpenzi wangu na sharti lile nililitekeleza.  Niliamini huenda ile ni ndoto ya kawaida tu wala haihusiani na ukweli wowote, kutokana na kutoelezwa chochote na mganga juu ya kupata ndoto yenye kiashirio.
“Vipi Masalu?” Sauti ya mpenzi wangu ilinishtua nikiwa katikati ya dimbwi la mawazo.
“Aah… safi tu,” nilijibu huku nikijitahidi kuficha kilicho moyoni mwangu.
“Safi, mbona umeamka na kukuona ukitupa mikono kama unazungumza na mtu kuna kitu gani kimekusibu?”
“Mmh! Kweli nimeona ndoto moja imenitisha sana.”
“Ndoto gani?”
“Nimeota nyumbani ndugu zangu wanalia baba akiwa amelala kitandani, lakini kitu cha ajabu amegeuka kiumbe cha ajabu chenye kutisha.”
“Sasa wasiwasi wako nini? hiyo si ndoto tu?”
“Huenda baba amekufa.”
“Masalu si ulielezwa atakufa kama tukikutana kimwili?”
“Ndiyo, hata mimi nashangaa.”
“Kwani mganga alikueleza nini juu ya njozi utakayoota?”
“Hakunieleza chochote.”
“Sasa wasiwasi wako nini?”
“Kwa vile baba hali yake ilikuwa mbaya, ndoto hii imenitisha sana.”
“Masalu acha kujitia presha bure, maisha ya baba yako yako mikononi mwako.”
“Mmh! Sawa, lakini niliingiwa na wasiwasi mkubwa.”
“Lala mpenzi.”
“Nashukuru kwa kunipa moyo.”
“Nipo hapa kwa ajili hiyo.”
“Asante mpenzi wangu kwa kunijali sina cha kukulipa.”
“Cha kunilipa baada ya kupona ni ndoa tu.”
“Omba jingine hilo umepata.
Niliagana na mpenzi wangu kila mmoja alilala, usingizi haukuchelewa kunichukua, haikuchukua muda mrefu njozi ilijirudia, tena safari hii niliwasikia wakilia huku wakitupia shutuma zao kwangu kuwa mimi ndiye chanzo cha kifo cha baba.
Nilishtuka tena kitandani na kuwasha taa, mpenzi wangu naye alishtuka na kuhoji kwa nini nimeamka tena.
“Masalu, vipi mpenzi wangu?”
“Mmh!” niliguna tu.
“Mbona sikuelewi?”
“Mmh! Ndoto bado inaning’ang’ania.”
“Umeota nini tena?”
“Bado kifo cha baba kinaendelea na safari hii nimewasikia mama na ndugu zangu wakinishutumu ndiye niliyesababisha.”
“Lakini bado itakuwa ni njozi tu kwa vile mawazo yako yote umeyahamishia huko.”
“Kwa hiyo nifanyeje?”
“Hebu iache njozi iishe wala usiamke.”
“Mmh! Ngoja nijaribu.”
Nilirudi kulala tena, ajabu nililala mpaka asubuhi bila kuota tena, mpenzi wangu ndiye aliyeniamsha.
“Masalu.”
“Naam.”
“Vipi upo sawa?”
“Nipo sawa, vipi?”
“Naona leo umelala sana.”
“Kwa muda huu ni saa ngapi?”
“Mmh! Ni saa tatu na nusu.”
“Ooh! Leo nimelala sana.”
“Inawezekana ni kutokana na kuamkaamka usiku kutokana na njozi ulizoota.”
“Na kweli.”
“Vipi uliota tena?”
“Sikuota, nimelala vizuri.”
“Unaona wasiwasi wako tu, njozi zingine hutokana  na mawazo ya mtu.”
“Ni kweli, lakini ziliniweka kwenye hali mbaya kwa vile kama kweli baba atakufa ndugu zangu hawatanielewa.”
“Wasikuelewe vipi?”
“Si nitaonekana mimi ndiye niliyemuua.”
“Masalu acha kujitoa akili, ulikwenda sehemu gani kumroga baba yako?”
“Sijaenda popote.”
“Sasa?”
“Si inaonesha kuwa uchawi umewarudia.”
“Hukuwaroga?”
“Ndiyo.”
“Sasa wewe unaogopa nini?”
“Mmh! Suala la kuua si la kawaida.”
“Wangekuua wewe lingekuwa la kawaida au umefurahia kuuawa kwa dada yako Monika?”
“Swali gani hilo, hujui nilivyoumizwa na kifo cha dada yangu?”
“Sasa inakuwaje unaogopa vifo vya watu mnajua kabisa hawana nia nzuri na wewe?”
“Basi tuachane na hayo, tuoge tukapate chai.”
Niliamka kitandani na kwenda kuoga, baada ya kuoga tulikwenda kupata kifungua kinywa kilichokuwa mlemle kwenye hoteli tuliyokuwa tumepanga.
Wiki ilikatika tukiwa tumejificha na mpenzi wangu, hata simu niliamua kuizima ili kuondoa usumbufu wa ndugu zangu. Siku moja asubuhi tukiwa mgahawani tukipata kifungua kinywa niliamua kuwasha simu. Utafikiri kuna mtu alikuwa akisubiri kwa hamu nilipowasha tu simu iliingia. Kuangalia ilionesha namba ya kaka yangu, niliiangalia kwa muda bila kupokea mpaka ikakatika. Haikupita muda simu iliita tena alikuwa dada nayo niliiangalia bila kuipokea.
“Masalu mbona hupokei simu?”
“Achana nao.”
“Kina nani?”
“Si hawa wapuuzi.”
ITAENDELEA

1 comment:

  1. umiteka bankuja kwayo hadithi hino. Pole kwayo masaibu hayo.

    ReplyDelete